TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MSIBA WA KANUMBA
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA)
kinaungana na wasanii wote nchini na Watanzania kwa ujumla kuombeleza kifo cha
msanii mahiri Steven Kanumba kilichotokea usiku wa kuamkia Jumamosi jijini Dar
es Salaam.
TASWA imeshtushwa taarifa za kifo cha Kanumba, hivyo tunatoa
pole kwa familia ya msanii huyo na wasanii wote wengine katika kipindi hiki
kigumu cha kuondokewa na msanii huyo. Kanumba atakumbukwa na waandishi wa
habari za michezo na burudani kutokana na ukaribu wake kwao na alikuwa na
ushirikiano wa kutosha pale alipoombwa kufanya hivyo, hali ambayo waandishi wa
habari za michezo na burudani nchini wataendelea kumbukumbuka.Mungu amuweke
mahali pema peponi.
B.PONGEZI KWA SIMBA KUINGIA 16 BORA
TASWA inatoa pongezi za dhati kwa timu ya Simba ya Dar es
Salaam baada ya kufanikiwa kuingia hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kuitoa ES Setif ya Algeria Ijumaa
iliyopita.
Tunaamini kusonga mbele kwa Simba ni hatua nzuri katika
kufikia mafanikio ya kweli ya mpira wa miguu hapa nchini, hivyo tunaamini kila
mdau wa soka atakuwa ameguswa kwa namna moja au nyingine kutokana na mafanikio
ya Simba.
Tunawasihi wachezaji wa Simba na viongozi pamoja na
mashabiki wa klabu hiyo, wasibweteke na mafanikio hayo badala yake waunganishe
nguvu ili waingie hatua inayofuata hatimaye watwae ubingwa maana hakuna
lisilowezekana chini ya jua.
WAANDISHI WALIOSHINDA TUZO
Kamati ya Utendaji ya TASWA inatoa pongezi za dhati kwa
waandishi wa habari za michezo walioshinda Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa
Habari (EJAT) zilizofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Waandishi hao ni Imani Mani aliyeshinda upande wa magazeti,
Anwar Mkama upande wa televisheni na Abdallah Majura upande wa redio, ambao
tunaamini juhudi za kazi zao zimefanikisha kupata tuzo hizo.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
08/04/2012