EL MAAMRY, NDOLANGA WATUNUKIWA URAIS WA HESHIMA
AGM ilipitisha pendekezo la kuwatunuku urais wa heshima wa
TFF, Alhaji Said Hamad El Maamry na Muhidin Ahamadi Ndolanga lililowasilishwa
na Mwenyekiti wa mkutano huo ambaye pia ni Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Alhaji El Maamry ambaye ni mjumbe wa heshima wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) alikuwa Mwenyekiti wa TFF wakati huo ikiitwa
Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) kuanzia mwaka 1973 hadi 1986. Alhaji
Ndolanga aliongoza FAT kuanzia mwaka 1993 hadi 2004.
BAJETI YA MWAKA 2012
Bajeti ya Mwaka 2012 ya sh. 7,246,628,650 kwa ajili ya
matumizi ya TFF ilipitishwa. Kwa mwaka 2012 TFF inatarajia kukusanya sh.
7,572,991,433 kupitia vyanzo mbalimbali.
Vyanzo hivyo ni viingilio vya uwanjani vinavyotarajiwa
kuingiza asilimia 22 ya mapato yote, udhamini (asilimia 74) na vyanzo vingine kama haki za matangazo ya televisheni, ada za ushiriki wa
timu katika mashindano mbalimbali, misaada kutoka FIFA na CAF ambayo kwa pamoja
vinatarajiwa kuingiza asilimia nne ya mapato yote.
UUZWAJI WA TIMU
Uuzaji wa timu linabaki kuwa suala la kisheria. Lakini TFF
imeweka utaratibu ufuatao; lazima Mkutano Mkuu wa klabu husika uidhinishe
uuzaji, na timu ikishauzwa inabaki katika mkoa husika.
MFUMO WA MASHINDANO
Kwa vile kuna tatizo la ligi mbalimbali kuwa fupi, hali
inayosababisha baadhi ya wachezaji katika madaraja ya chini kucheza ligi zaidi
ya moja katika msimu mmoja, mfumo wa ligi/mashindano utaangaliwa upya.
Mfumo uliopo sasa uliwekwa kwa ajili ya kuvutia uwekezaji
katika mpira wa miguu ambapo mwekezaji anaweza kuanzisha timu, na ndani ya
miaka mitatu ikacheza Ligi Kuu. Pili, ilikuwa ni kuondoa mlolongo mrefu wa
ligi, na kuwafanya wanachama wa TFF (mikoa) nao kuendesha ligi zao mikoani.
Ijulikane kuwa ligi za mikoa (regional leagues) zinachezwa.
Kwa sababu TFF inaendeshwa kwa mfumo wa shirikisho (federation), nia ni
wanachama wa federation nao kuwa na majukumu ya kusimamia na kuendesha ligi,
kwa vile TFF haiwezi kusimamia ligi zote.
MAREKEBISHO YA KATIBA
Mkutano Mkuu wa TFF umepitisha marekebisho ya Katiba katika
maeneo mawili; moja ni kuanzisha Baraza la Wadhamini ambalo linatakiwa kuwa na
wajumbe wasiopungua watatu na wasiozidi watano.
Marekebisho mengine ni kuongeza idadi ya kanda kutoka kumi
na moja za sasa hadi 13. Marekebisho hayo yamefanyika kutokana na Serikali
kuongeza mikoa mipya ya kijiografia.
Kanda mpya sasa zitakuwa Kagera/Geita, Arusha/Manyara,
Kilimanjaro/Tanga, Katavi/Rukwa, Njombe/Ruvuma, Dodoma/Singida, Dar es Salaam ,
Shinyanga/Simiyu, Mwanza/Mara, Lindi/Mtwara, Kigoma/Tabora, Mbeya/Iringa na
Pwani/Morogoro.
Ukiondoa mamlaka ya uteuzi aliyonayo Rais kwa mujibu wa
Katiba ya TFF, wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji huchaguliwa kwa kanda.
HESABU ZILIZOKAGULIWA
Mkutano Mkuu ulipitisha hesabu zilizokaguliwa za mwaka 2010
(Audited Accounts) , na pia kuiteua kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya TAC
Associates kuwa mkaguzi wa hesabu za TFF kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
KANUNI ZA NIDHAMU, MAHAKAMA YA USULUHISHI
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Rais Tenga
aliwaambia wajumbe kuwa Kanuni za Nidhamu (Disciplinary Code) za TFF na uundaji
wa Mahakama ya Usuluhishi (Arbitration Tribunal) ya TFF ambacho ndicho kitakuwa
chombo cha juu cha kutoa haki kwa masuala ya mpira wa miguu nchini vitakamilika
mwaka huu.
Pia TFF itaendelea kutafuta wadhamini kwa ajili ya timu za
Taifa za vijana na wanawake, itaendelea kuendesha semina na makongamano katika
nyanja mbalimbali za mpira wa miguu, kutengeneza mtaala wa academy na
kutengeneza mpango wa maendeleo (Comprehensive Plan) baada ya ule wa awali
kumalizika mwaka huu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)