LICHA ya kutakiwa kujiweka kando kwenye uongozi baada ya
timu kufanya vibaya katika ligi kuu soka Tanzania bara, uongozi wa klabu ya
soka ya Yanga umewaomba wanachana kuwa na subira mpaka ligi itakapomalizika.
Hatua hiyo inafuatia wanachama wa klabu hiyo kuutaka uongozi
wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake Lloyd Nchunga ujiuzulu baada ya timu kupoteza
mwelekeo kwenye ligi hiyo na hatimaye kushindwa kutetea ubingwa wake.
Katibu mkuu wa Yanga
Selestine Mwesiga ameiambia mamapipiro blog kwamba, kujiuzulu kwa viongozi si suluhisho la timu kufanya
vibaya kwenye ligi hiyo ambayo inaelekea ukingoni.
Alisema kufanya vibaya kwa timu hiyo huenda kunachangiwa na
mambo tofauti hivyo kuuutupia lawama uongozi kujiondoa madarakani si suluhisho
hivyo ligi itakapomalizika watakaa na kujua tatizo ni nini.
“Unajua kuteleza kuna sababu nyingi labda tatizo ni katika
idara ya ufundi, ama utawala na hata mfumo mzima wa ligi sasa kutaka uongozi
kujiuzulu haiwezi kusaidia lolote, kikubwa ni kusubiri ligi imalizike
kwanza,”alisema.
“Si utamaduni wetu kujiuzulu wakati ligi haijaisha, tunajua
wapenzi wetu wanaumia sana
kutokana na timu kufanya vibaya lakini nawaomba wanachama wawe na subira na
tutahakikisha timu inafanya vema katika michezo yake iliyosalia kwenye
ligi,”alisema Katibu huyo.
Katibu huyo aliongeza kwamba wanachama wa Yanga wanahaki ya
kulalamika mwenendo mzima wa timu hiyo kwani ni wajibu wao lakini wanapaswa
kukumbuka kuwa uongozi huohuo muda mfupi baada ya kuingia madarakani timu yake
ilitwaa mataji matatu.