Jakaya akihani wafiwa |
POMBE kali (Whisky) aina ya
Jacky Daniel, imetajwa kama chanzo cha kifo cha mwigizaji nyota wa filamu
nchini, Steven Charles Kanumba aliyefariki usiku wa kuamkia jana nyumbani
kwake, Sinza, Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Kinondoni, ACP
Charles Kenyela amesema leo kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha hivyo, lakini
bado wanaendelea na uchunguzi zaidi, ili kujua zaidi.
ACP Kenyela amesema kwamba
Kanumba wamefanikiwa kumuhoji mtuhumiwa wa kwanza katika tukio hilo, Elizabeth
Michael ‘Lulu’ na katika maelelezo yake amekanusha kumsukuma Kanumba.
Vyombo vingi vya habari
vilimnukuu ndugu wa Kanumba, Sethi jana akisema kwamba Lulu alimsukuma mwigizaji
mwenzake huyo katika ugomvi wao wa wivu wa kimapenzi hadi akaanguka na kufariki
dunia.
Akizungumza kutokana na maelezo
ya Lulu, Kamanda huyo alisema kwamba; ugomvi wao ulitokana na Kanumba kutaka
kumdhibiti Lulu wakati akizungumza na simu.
“Kanumba aliamua kumfuata Lulu
nje huku akifoka kwa sauti, akitaka aelezwe kwa nini alitoka nje kupokea simu,
huku akimtuhumu kuwa huenda alikuwa akizungumza na mwanaume mwingine.
Baada ya Lulu kuona Kanumba
anamfuata, aliamua kukimbia kutoka nje ya geti, lakini kabla hajafanikiwa
kufungua geti, Kanumba alimkamata na
kumrudishwa ndani. Kanumba akiwa amemshikilia, waliingia wote chumbani na
kufunga mlango. Sasa haijulikani nani aliyefunga mlango, ingawa maelezo ya
Lulu, anadai kuwa aliyefunga mlango ni Kanumba,”alisema Kamanda huyo.
Akiendelea kumnukuu Lulu,
Kamanda huyo anasema; “Baada ya Kanumba kufunga mlango, alimuona akilegea na
kujigonga kisogo chake kwenye ukuta wa chumba hicho kabla ya kuanguka
chini,”alisema.
Alisema uchunguzi wa tukio zima
ukikamilika, hatua inayofuata ni kumpeleka Lulu mahakamani kama mtuhumiwa wa
mauaji.
Wakati huo huo: mchana wa leo,
rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alifika nyumbani
kwa marehemu, Sinza Vatican kuhani msiba.
Mama wa marehemu anatarajiwa
kuwasili leo- ili kwa pamoja na Kamati ya Mazishi waamue kuhusu mwili wa
marehemu uzikwe wapi.
Kamati ya Mazishi, inataka
kumshawishi mama huyo anayetokea Bukoba, akubali Kanumba azikwe Dar es Salaam.
Mwili wa marehemu unatarajiwa
kuagwa Jumanne katika viwanja vya Leaders, Dar es Salaam na baada ya hapo ndipo
litafuatia zoezi la mazishi.
HISTORIA YAKE:
Steven Charles Kanumba alizaliwa
Januari 8, mwaka 1984, mkoani Shinyanga, kabla ya umauti kumfika Aprili 6,
mwaka 2012.
Elimu ya msingi alipata katika
shule ya Bugoyi, Shinyanga na baadaye akajiunga na sekondari ya Mwadui, kabla
ya kuhamia Dar Christian Seminary.
Baada ya kumaliza Kidato cha Nne
Dar Christian, Kanumba alijiunga na sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam pia
kwa elimu ya Kidato cha Tano na Sita.
Ni wakati huo akiwa Jitegemee,
Kanumba alianza shughuli za sanaa katika Kundi la Kaole Sanaa Group la
Magomeni, Dar es Salaam.
Baada ya kukomaa Kaole, Kanumba
aliamua kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya filamu na hadi anakutwa na umauti
alikuwa mwigizaji anayefahamika Afrika nzima.
Ameshirikiana na wasanii wakubwa
duniani kama Ramsey Nouah wa Nigeria na amefanya kazi na mastaa wengine kadhaa
wa Nigeria.
Miongoni mwa filamu ambazo
alifanya ni Dar To Lagos, She is My Sister, Ancle JJ, Oprah, Tufani, Johari,
Gharika, Baragumu, Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Cross My Sin, Village
Pastor, Family Tears na kadhalika.
Hivi karibuni, alikaririwa
akisema atagombea Ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
Kanumba atakumbukwa na wengi
sana kwa ucheshi wake- upole na ushirikiano mzuri na wenzake katika kazi.
Kifo cha Kanumba ni pigo katika
tasniya ya filamu Tanzania. Taifa limempoteza mtu ambaye alikwishaanza
kuitangaza vema nchi kupitia sanaa hiyo na ambaye angetarajiwa kuitangaza zaidi
katika anga za kimataifa zaidi kupitia sanaa hii.
Nigeria sasa wanajua Tanzania
kuna filamu. Nchi nyingi za Afrika zinajua sasa na hii sehemu ya kazi nzuri ya
Kanumba.
Mwenyewe aliwahi kukaririwa
alifika hadi Hollywood, Marekani, ambayo ni ‘makka’ ya wacheza filamu. Kwa sasa
mwili wa marehemu upo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin.
kumbe alikua anakunywa pombe!!si mara kadhaa alikua akidai hanywi huyu au alikua akinywa akiwa na kazi maalum?
ReplyDeletekweli huu msiba utafunua mambo mengi.
Otherwise,Poleni sana wafiwa
mdau wa bomba,revere,massachussetts,usa