UONGOZI wa Yanga umesema watachukua hatua za kisheria iwapo kocha wao mkuu Kostadin Papic atavunja mkataba na klabu hiyo.
Hatua hiyo inafuatia Papic kuaga rasmi kwa mashabiki wa klabu hiyo jana na kusema kuwa anaondoka Aprili 26 huku akiudai uongozi mshahara wake wa miezi miwili.
Katibu Mkuu wa Yanga Mwesigwa Selestine aliiambia mamapipiro blog kwamba mkataba wa kocha huyo unamalizika baada ya msimu huu wa ligi kuisha lakini anashangazwa na taarifa za kocha huiyo kutishia kuondoka.
Alisema uongozi bado unamtambua Papic kama ni kocha wao na anaamini Papic anazifahamu ipasavyo sheria za mikataba.
"Nimeona katika baadhi ya vyombo vya habari kama Papic ameaga rasmi, sasa napenda kuweka wazi kwamba mkataba wa Papic utaisha msimu utakapomalizika, kama ataamua kuondoka ni wazi atakuwa ameuvunja hivyo tutafuata taratibu za kisheria,"alisema.
Aidha, katibu huyo alikanusha kocha huyo kudai mshabara wa miezi miwili ambapo alisema kwamba mwezi Machi alichukua advance ya mshahara wake,huku mshahara wa mwezi huu bado hajalipwa.
Mwesigwa aliongeza kwamba pamoja na malalamiko hayo kocha huyo amekuwa akipatiwa huduma zote nje ya mshahara wake ikiwemo malazi, usafiri, matibabu, chakula, mawasiliano na mengine mengi .
Iwapo kocha huyo kutoka Serbia ataondoka nchini itakuwa ni mara yake ya pili kutoroka ambapo alifanya hivyo mwaka juzi kabla ya baadhi ya wadau kumrejesha tena mwaka jana.