Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ambaye pia mjumbe wa
Mkutano Mkuu wa TFF akiwakilisha klabu za Mkoa wa Dar es Salaam , Mohamed Bhinda (pichani)aliwaomba radhi
wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kitendo cha wachezaji wake kumpiga mwamuzi Israel
Nkongo kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10
mwaka huu.
Pia alimuomba Rais wa TFF, Leodegar Tenga kutoa msamaha wa
adhabu ya kulipa faini iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa wachezaji
wawili wa Yanga ambao mpaka sasa hawajalipa faini hiyo.
Rais Tenga alimshukuru Bhinda kwa ujasiri alioonesha wa
kuomba radhi mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kitendo kile.
Aliongeza kuwa kwa vile yeye ni muumini wa kanuni, na adhabu hizo zimetolewa
kwa mujibu wa kanuni hawezi kutoa msamaha, hivyo wachezaji hao walipe faini
hizo.
Pia Rais Tenga alisema binafsi haziingilia kamati za TFF
katika uamuzi ambao zinafanya kwa vile zina watu waadilifu, na angekuwa yeye
binafsi ndiye anayetoa adhabu, angetoa adhabu kali zaidi kwa vile vitendo vya
kupiga waamuzi havikubaliki katika mchezo wa mpira wa miguu.