YANGA YA\ZINDUKA, YAUA 3-1 TAIFA

Kikosi cha Yanga

KLABU ya Yanga, jioni hii imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Polisi Dodoma ambayo imekwishashuka Daraja.


Mabao ya Yanga yametiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Davies Mwape mawili na Idrisa Rashid moja.
Ushindi huo, unaifanya Yanga sasa itimize pointi 46 baada ya kucheza mechi 24, ikiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo, nyuma ya Azam FC yenye pointi 50, ambayo kesho inacheza na Mtibwa Sugar.
Azam ikishinda kesho itafikisha pointi 53, ambazo haziwezi kufikiwa na Yanga- maana yake itakuwa imejihakikishia kucheza michuano ya Afrika mwakani ikiungana na Simba, inayoongoza ligi hiyo kwa pointi zake 56.
Yanga ilipoteza nafasi ya kutetea ubingwa baada ya kupoteza pointi tisa m fululizo katika mechi zake tatu zilizopita, dhidi ya Coastal Union ya Tanga, Toto African ya Mwanza na Kagera Sugar ya Bukoba.
Licha ya kuifunga Coastal 1-0 kwa bao pekee la Mwanasoka Bora wa Uganda, Hamisi Kiiza 'Diego', Yanga ilipokonywa pointi tatu na Kamati ya Ligi Kuu, kwa kosa la kumtumia beki Nadir Haroub Ally 'Cannavaro' aliyekuwa bado anatumikia adhabu ya kadi nyekundu.
Ikiwa haijamaliza machungu ya kupoteza pointi hizo, Yanga ilikwenda kufungwa na Toto mabao 3-2 mjini Mwanza. Toto ni timu ambayo inamilikiwa na tawi la Yanga mjini Mwanza na mara nyingi mechi baina ya timu hizo huchukuliwa kama zipo kwa ajili ya Yanga kushinda, lakini msimu huu wakiwa wanapigania kuepuka kushuka daraja, Wana Kishamapanda waliwageuzia kibao baba zao waliokuwa wakisaka japo nafasi ya pili.
Ikitarajiwa labda itazinduka mjini Bukoba, Yanga ilikung'utwa bao 1-0 na Kagera Sugar, ambayo inayopogana kuepuka balaa la kushuka daraja.

Post a Comment

Previous Post Next Post