WAKATI funga pazia la
Ligi Kuu bara likisogezwa mbele kwa siku moja, watani Simba na Yanga wamepokea
uamuzi huo kila moja kwa mtazamo wake.
Awali wakongwe hao
walikuwa waumane kesho kwenye Uwanja wa Taifa, lakini kutoka na uamuzi wa
Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
sasa wataumana Jumapili.
Klabu zote, licha ya
kukubali kushuka dimbani Jumapili, zimeelezea kusikitishwa na uamuzi huo wa
kusogezwa mbele, kwani umewaharibia programu zao na kuongeza gharama za
uendeshaji, huku Yanga ikitaka ilipwe fidia.
Akizungumza kwa njia ya
simu jana, msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga ‘Mr. Liverpool’, alisema kuwa
ingawa hawajazifurahia taarifa hizo, lakini wako tayari kushuka dimbani.
Alisema kusogezwa mbele
kwa siku moja zaidi kwa mechi hiyo, kutawaongezea gharama kwa kuwa timu yao iko kambini visiwani Zanzibar , lakini hawana kinyongo.
Aliongeza kuwa kusogezwa
mbele kwa mechi hiyo, kutawanyima pia muda wa kutosha wa kupumzika,
wanapojiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya Al Ahli Shendi ya Sudan , katika
Kombe la Shirikisho (CAF).
Kwa upande wa Yanga, wameitaka
TFF kugharimia gharama za siku moja iliyosogezwa.
Mwenyekiti wa Yanga,
Lloyd Nchunga, aliiambia Tanzania Daima kuwa kutokana na jinsi walivyokuwa
wamejipanga kwa gharama za kuiweka timu kambini, inawagharimu kuanza kutafuta
fedha za ziada na kuitaka TFF kubeba jukumu hilo.
Nchunga alisema kikosi
chao kiko kambini mjini Bagamoyo kwa ajili ya maandalizi na kuwa walikuwa
wamejipanga na kujua kambi yao inamalizika kesho
na kurejea jijini asubuhi tayari kwa pambano hilo .
Alifika mbali zaidi na
kubainisha kuwa endapo TFF watashindwa kugharamia siku hiyo moja, basi wawalipe
deni lao ambalo wanawadai, zaidi ya sh milioni 9, ili waweze kuhakikisha
wanamudu kuwagharimia wachezaji wao kambini, ndani ya siku hiyo moja.
Akizungumzia madai hayo, Katibu
Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema wao sio ambao wamesogeza mechi hizo mbele,
bali ni moja ya chombo cha shirikisho hilo ,
ambacho ni Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ambayo ndiyo iliyopendekeza mechi
hizo kusogezwa.
“Mbona tulipokuwa
tunasogeza mechi nyingine ama kuzirudisha nyuma, walikuwa hawalalamiki wala
kusema kitu kama hicho na wanakuja kusema kwa
sasa, sisi tumekisikiliza chombo chetu na ndiyo maana tukatangaza hivyo,” alisema
Osiah.