Ngorongoro Heroes imewasili salama
hapa Khartoum jana saa 4 usiku kwa ajili ya mechi ya michuano ya
Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 dhidi ya Sudan. Mechi hiyo
itachezwa Jumamosi kuanzia
saa 2.00 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum ambao ni wa nyasi bandia, na
hakutakuwa na kiingilio kwa
watazamaji.
Awali Ngorongoro Heroes ilitarajiwa kuwasili saa 2.10 usiku, lakini ndege
iliyokuwa ipande Nairobi kuja
hapa ilichelewa kuondoka kwa saa moja na nusu kutokana na hali ya hewa
kutokuwa nzuri katika Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kulikosababishwa na mvua
kubwa iliyokuwa ikinyesha uwanjani hapo.
Mara baada ya kuwasili Taka Hotel ambapo imefikia, Ngorongoro Heroes
ilifanya mazoezi ya saa moja
kuanzia saa 4.30 usiku kwenye Uwanja wa Khartoum ambao ndiyo utakaotumika
kwa mechi dhidi ya
Sudan. Ngorongoro Heroes ilishinda mchezo wa kwanza mabao 3-1 kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es
Salaam.
Hoteli ya Taka ndipo pia timu ya El Merreikh ya hapa Sudan imeweka kambi
yake kujiandaa kwa mechi ya
marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC).
El Merreikh ililala mabao 2-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini
Lubumbashi.
Kwa mujibu wa kocha Kim Poulsen, wachezaji wote wako katika hali nzuri na
kikosi kitakachoanza kwenyemechi hiyo kitajulikana kesho (Ijumaa) baada ya mazoezi ya mwisho
yatakayofanyika saa 2 usiku kwenyeUwanja wa Khartoum.
Wachezaji walioko kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes ni Aishi Manula,
Ramadhan Singano, Hassan
Dilunga, Frank Damayo, Frank Sekule, Issa Rashid, Hassan Ramadhan, Saleh
Malande, Said Zege, Emily
Mugeta, Jerome Lambele, Samir Ruhava, Simon Msuva, Thomas Ulimwengu,
Atupele Green, Dizana
Yarouk, Jamal Mroki na nahodha Omega Seme.
Mwamuzi Aden Abdi Djamal wa Djibouti ndiye atakayechezesha mechi hiyo.
Djamal atasaidiwa na
Wadjibouti wenzake Egueh Yacin Hassan, Bogoreh Salime Fahan na Aden Ali
Farah. Waamuzi hao
watawasili kesho (Ijumaa) saa 8 mchana
kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakati Kamishna wa mechi hiyo
Patrick Naggi kutoka Kenya atawasili leo (Alhamisi) saa 2.10 usiku kwa
ndege ya Kenya Airways.
Iwapo Ngorongoro Heroes itafanikiwa kuitoa Sudan itacheza mechi ya raundi
ya pili dhidi ya Nigeria. Mechi
ya kwanza itchezwa Julai 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya
marudiano itakuwa kati ya Agosti 10
na 12 mwaka huu.
Ikifanikiwa kuitoa Nigeria, Ngorongoro Heroes itacheza mechi ya raundi ya
tatu na mshindi kati ya Afrika
Kusini na Congo Brazzaville. Mechi ya kwanza itakuwa ugenini kati ya
Septemba 21 na 23 mwaka huu
wakati ya marudiano itakuwa nyumbani Oktoba 6 mwaka huu.
Boniface Wambura,
Khartoum, Sudan
Mei 3, 2012