WANACHAMA
wapatao 700 wa klabu ya Yanga, jana kwa kauli moja walitangaza kuung’oa
madarakani uongozi wa Lloyd Nchunga katika mkutano uliofanyika kwenye Uwanja wa
Kaunda, jijini Dar es Salaam.
Mkutano
huo ulioratibiwa na Baraza la Wazee kwa kushirikiana na vijana, ulihamia kwenye
uwanja huo kutokana na idadi kubwa ya wanachama waliojitokeza kuamua hatima ya
klabu yao.
Katika
mkutano huo uliodumu kwa saa mbili, kuanzia majira ya saa 6 hadi 8 mchana, muda
ulivyokuwa ukisogea, ndivyo wanachama walivyokuwa wanaongezeka.
Ingawa
mkutano huo ulianza na wanachama wapatao 556, lakini hadi unafungwa, walikuwa
wamefikia 700, wote kwa pamoja wakiridhia kuuweka kando uongozi wa Nchunga.
Baada
ya mkutano huo kufunguliwa na dua na sala, Katibu wa Wazee, Ibrahim Akilimali,
alitoa maneno machache kuelezea udhaifu wa uongozi wa Nchunga tangu uingie
madarakani Julai 18, 2010.
Akilimali
aliwaeleza wanachama kuwa, kutokana na mambo kutokwenda sawa katika klabu yao, ndiyo maana waliamua
kuchukua jukumu la kuitwaa timu kuelekea mechi ya Simba.
Alisema,
sababu ya wao kufikia hatua hiyo, ni wachezaji kukosa ari ya kucheza kutokana
na matatizo ya uongozi wa Nchunga ikiwemo kutolipwa mishahara, hivyo kuishi kwa
dhiki kubwa.
“Ndugu
zangu, tulitaka tuchukue timu kwa nia ya kuepuka kufungwa na Simba, awali
Nchunga aliridhia, lakini baadaye aligeuka, nasi tukajiweka kando na matokeo
yake umeyaona (Yanga ilichapwa mabao 5-0),” alisema Akilimali akishangiliwa na
wanachama wenzake.
Alisema
hatua ya kumtaka Nchunga akae kando, ni kutokana na kushindwa kuongoza kwani
kuna hatari ya klabu hiyo kuingia kwenye madeni yatakayogharimu uhai wake.
Akilimali
alisema, udhaifu na matatizo ya uongozi wa Nchunga, yanathibitishwa na wajumbe
wa Kamati ya Utendaji walioamua kumsusia klabu hiyo.
Alisema,
miezi michache tangu kuingia madarakani, makamu wake, Davis Mosha alijiuzulu
akifuatiwa na wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji hivi karibuni, hivyo hafai
kubaki Yanga.
Mbali
ya Mosha, wengine walioachia ngazi, ni Seif Ahmed, Ally Mayay, Edgar Chibula na
Abdallah Bin Kleb, ambao wote walifanya hivyo kutokana na matatizo yaliyomo
kwenye uongozi wa Nchunga.
Kuhusu
fedha za kuendesha timu, Akilimali alisema tayari wameahidiwa kupewa sh mil 750
na watu wenye mapenzi na klabu hiyo, na kwamba kuna mfanyabiashara mmoja
ameahidi kutoa sh mil 250, hivyo kufikia sh bil 1.
Kati
ya waliopewa nafasi ya kusema machache, ni kipa wa zamani wa timu hiyo, Hamisi
Kinye na beki Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, ambao waliushutumu uongozi wa
Nchunga kwa usajili mbovu.
Kwa
mujibu wa Katiba ya Yanga, iwapo theluthi ya wanachama watajiorodhesha na kutia
saini zao, maamuzi watakayofikia, ni halali.
Baada
ya kupitisha uamuzi huo, Akilimali alisema watawasilisha orodha ya wanachama
waliojiorodhesha kushiriki mkutano huo kwa Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo
Wilaya ya Ilala kuomba uchaguzi mkuu.
Tangu
Yanga ipoteze mwelekeo wa ubingwa wa Ligi Kuu, kumekuwa na harakati za kuung’oa
uongozi wa Nchunga kwa hoja ya kushindwa kazi, huku wachezaji na makocha
wakilia kutolipwa mishahara.