KOCHA wa Riadha wa Timu ya Tanzania inayotarajiwa kushiriki mashindano ya Olimpiki London, Julai 27 hadi Agosti 12 mwaka huu, Zakaria Gwandu, ameelezea kusikitishwa na kushangazwa kwa mchezaji Faustine Mussa kutojiunga na wenzake kambini, Mkuza Kibaha.
Akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi jana, Gwandu, alisema, wakati timu ikitarajiwa kuondoka nchini Julai 8 mwaka huu, Mussa ambaye ni mwajiriwa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), ndiye pekee hawajatia mguu kambini hapo, jambo linalomweka katika wakati mgumu wa kutekeleza programu zake.
“Kwa kweli sielewi kinachoendelea kuhusiana na mchezaji huyu Faustine Mussa, sijui tatizo ni kwa mchezaji au mwajiriwa wake, kwani barua ya kuombewa ruhusa Chama cha Riadha (RT), kilikwisha ituma kwa mwajiri wake muda mrefu, lakini mchezaji hadi sasa hajatokea kambini,” alilalamika Kocha huyo.
Timu ya riadha itakayoshiriki michezo ya Olimpiki London nchini Uingereza, inaundwa na wachezaji wanne, Zakia Mrisho, Samson Ramadhani, Msenduki Mohamed na Faustine Mussa, ambaye bado hajaripoti kambini.