TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Simba kushiriki Kombe
la Tanzania
KLABU ya Simba inapenda kutangaza kuwa itashiriki katika
michuano ya Kombe la Tanzania
(Urafiki) iliyopangwa kuanza visiwani Zanzibar Jumatatu ijayo.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange,
maamuzi ya kushiriki katika mashindano hayo yamefikiwa baada ya majadiliano
baina ya uongozi, benchi la ufundi na Kamati ya Ufundi ya Simba.
“Tumeamua kushiriki kwa sababu tumeona haitakuwa vema
kufanya hivyo wakati watu wa Zanzibar
wametupa heshima kubwa ya kutualika kwenye michuano hii. Kombe la Tanzania
lina maana kubwa kwa sasa kutokana na hali halisi ya kisiasa na kijamii iliyopo
visiwani humo kwa sasa,” alisema.
Makamu alisema zaidi ya kushiriki michuano hiyo, Simba pia
itatumia fursa hiyo kuweka kambi maalumu kwa ajili ya kujiandaa na Kombe la
Kagame lililopangwa kufanyika kuanzia Julai 14 mwaka huu.
Pia, alisema Simba itatumia ziara hiyo kupeleka kombe la
Ligi Kuu ya Vodacom kwa wana Simba wa Zanzibar
ambao walichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa ubingwa Vodacom na pia.
“Tusisahau pia kwamba kabla ya kucheza mechi yetu ya mwisho
dhidi ya watani wetu wa jadi Yanga ambayo tulishinda kwa idadi ya mabao 5-0,
Simba ilikwenda kuweka kambi Zanzibar ,”
alisema Kaburu.
Simba itaanza
michuano hiyo siku ya Jumatatu ambapo itacheza na Mafunzo ya Zanzibar katika pambano lililopangwa
kufanyika usiku. Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Jumatatu jioni lakini
imesogezwa mbele hadi Jumatatu usiku.
Jumla ya timu nane zinashiriki katika michuano hiyo ambapo
Waekundu wa Msimbazi wapo katika kundi A lenye timu za Simba, Azam, Mafunzo na
timu ya soka ya taifa ya vijana ya Zanzibar
wenye umri wa chini ya miaka 23 (Karume Boys).