MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba Mganda Emmanuel Okwi
hatoshiriki na timu yake katika michuano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na
Kati maarufu kama ‘Kombe la Kagame’ inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai 14
jijini Dar es Salaam.
Simba itaanza michuano hiyo julai 16 kwa kukwaana na URA
ya Uganda, mchezo utakaopigwa kuanzia saa 10.00 jioni kwenye uwanja wa Taifa.
Okwi atakosa michuano hiyo kufuatia nyota huyo kupata ofa
ya kufanya majaribio katika vilabu tofauti nje ya nchi ambapo atautumia mwezi
huo katika zoezi hilo.
Kiongozi mmoja wa Simba amesema leo kwamba Okwi anatarajia kuanza
safari yake ya majaribio Julai 4 ambapo ataelekea nchini Italia.
Alisema kuwa mbali na Itali, nyota huyo anayekipiga pia
timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ amepata ofa ya kucheza nchini Ujerumani na
Poland.
“Kama hatofuzu majaribio nchini Italy atakwenda Ujerumani
ambapo kuna timu moja imemtaka afanyiwe vipimo tu na kujiunga…kama vipi
atakwenda Poland kazi imebaki kwake kuamua,”alisema kiongozi huyo.
Aidha, Simba inaendelea na maandalizi yake ya michuano ya
Kagame ambapo kesho itashuka katika dimba la Taifa kukipiga na mabingwa wa
Uganda, Express.
Ofisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema leo kwamba maandalizi kwa ajili ya mchezo huo yamekamilika ambapo Simba itashusha
nyota wake wapya iliyowasajili sambamba na wale wa zamani.
Alisema mchezo huo ni muhimu kwao kwani kocha ataweza
kujua kiwango ilichofikia kikosi chake ambacho kimekuwa kikijinoa kwa majuma
kadhaa.
Kamwaga aliongeza kuwa timu hiyo itaelekea Visiwani
Zanzibar kwa ajili ya kambi maalum sambamba na kushiriki kombe la Tanzania
‘Urafiki’ lililoanza kutimua vumbi jana.
Jumla ya timu nane zitashiriki katika michuano hiyo
ambapo Simba ipo kundi A pamoja na Azam,
Mafunzo na timu ya soka ya taifa ya vijana ya Zanzibar wenye umri wa chini ya
miaka 23 (Karume Boys) ambapo itaanza michuano kesho usiku kwa kucheza na
Mafunzo ya Zanzibar .