Uongozi wa Twiga Stars umekana kuwepo vitendo vyovyote vya kinyume na maadili kwa wachezaji wa timu hiyo ambayo hivi karibuni ilitolewa kwenye mechi za mchujo za michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC).
Wakizungumza na waandishi wa habari leo (Julai 2 mwaka huu), Meneja wa Twiga Stars, Furaha Francis na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Charles Boniface Mkwasa wamesema hakuna vitendo vya aina hiyo.
Mkwasa amesema alikaririwa vibaya kuhusu suala hilo wakati akiwa kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha Star Tv kutokana na swali alilokuwa ameulizwa kuhusiana na vitendo hivyo.
“Ukifuatilia mahojiano yangu na Star Tv mimi sikusema kuwa kuna vitendo hivyo. Tatizo nadhani lilianzia kwa magazeti yaliyonukuu kupitia Star Tv, na wala kujiuzulu kwangu hakukuhusiana na hilo, nimewajibika kama kocha kutokana na kutolewa na Ethiopia,” amesema Mkwasa.
Naye Furaha Francis amesisitiza kuwa hakuna vitu vya aina hiyo katika timu hiyo, na kama kuna mtu ana ushahidi na hilo ni bora akauonesha badala ya kuzungumzia uvumi kuliko ukweli.
“Ukweli ni kwamba si sisi na wachezaji tu ambao hatukufurahishwa kutolewa na Ethiopia, wapo Watanzania wengi ambao hawakufurahishwa na matokeo yale. Twiga Stars si timu ya kudumu, haikai na wachezaji kwa muda wote, kila mchezaji ana timu yake.
“Madai yanayoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu vitendo hivyo yametuchafua sana. Tunaomba kama kuna mtu ana ushahidi na hilo atueleze kuliko kuendelea kutuchafua,” amesema.