1 Julai, 2012 - Saa 21:46 GMT
Uhispania waliandikisha historia kwa maarifa ambayo sio rahisi kuiga, kwa kuifunga Italia magoli 4-0 katika fainali ya Euro 2012 usiku wa Jumapili, mjini Kiev, Ukraine.
Licha ya mchezo mzuri wa Italia, vijana wa meneja wa Uhispania, Vicente del Bosque walithibitisha kwamba kimataifa wanaweza kujigamba wao ndio wenye mchezo bora zaidi duniani, kwa kuzingatia namna walivyoichezea timu ya Italia, na kuwalazimisha kusalimu amri.
David Silva aliifungia Uhispania bao la kwanza, na kabla nusu ya kwanza ya mchezo kumalizika, mchezaji mpya wa Barcelona, Jordi Alba aliandikisha bao la pili, baada ya kukimbia kwa kasi na kumalizia kwa ustadi kabisa.
Ingawa Italia walikuwa na upungufu wa mchezaji mmoja, baada ya kumpoteza mchezaji wa zamu wa tatu Thiago Motta baada ya kujeruhiwa, walicheza kwa bidii, lakini wataalamu wa kandanda kwa upande wa kupokezana mpira, Uhispania, waliwadunisha kabisa.
Fernando Torres aliingia kama mchezaji wa zamu, na akafanikiwa kuubadilisha mchezo, na akiandikisha bao la tatu la Uhispania, kabla ya mwenzake katika klabu ya Chelsea, Juan Mata, kuandikisha bao la nne na la mwisho la Italia, na ambalo bila shaka liliwavunja moyo kabisa mashabiki wote wa Italia.
Mchezo huo bila shaka umeyazima matamshi ya baadhi ya watu ambao awali walimlazimu kocha wa Uhispania Del Bosque na wachezaji wake kujitetea katika mkutano na waandishi wa habari, kabla mechi ya fainali kuanza, kwamba mchezo wao katika mashindano ya Euro 2012 umekosa msisimko.
Lakini usiku wa Jumapili mambo yalikuwa tofauti.
Maarifa yote yaliyowawezesha kuwa mabingwa wa Euro 2008 na vile vile Kombe la Dunia la mwaka 2010 nchini Afrika Kusini yalijitokeza.
Ilikuwa ni fainali ambayo ilimvunja moyo kabisa kocha wa Italia, Cesare Prandelli, lakini bila shaka haikuwa fedheha kushindwa na timu yenye maarifa ya hali ya juu kiasi hicho.
Italia itaweza kujivunia namna ilifika katika fainali, licha ya kushindwa kwa magoli mengi na timu ambayo ilikuwa ni wazi imo katika kiwango cha pekee.