Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) imeahidi ushindi kwenye mechi yake dhidi ya Nigeria (Flying Eagles) itakayochezwa kesho (Julai 29 mwaka huu).
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa vijana wenye umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Algeria itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika leo (Julai 28 mwaka huu) ofisi za TFF, Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Jakob Michelsen na nahodha wake Omega Seme wamesema timu yao iko tayari kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Kenya.
Michelsen amesema timu yake imepata mechi mbili za kujipima nguvu dhidi ya Rwanda, lakini pia aliishuhudia Flying Eagles ikicheza mechi ya kirafiki na Rwanda (Young Amavubi) uliofanyika Julai 24 mwaka huu jijini Kigali.
“Timu iko vizuri na wachezaji kama Frank Domayo, Simon Msuva na Ramadhan Singano ambao pia wanachezea timu A (Taifa Stars), hivyo uzoefu wao ni muhimu kwa mechi ya kesho.
“Nigeria ni mabingwa watetezi wa michuano hii kwa hiyo tunatarajia upinzani mkubwa, lakini tumejiandaa kwa hilo. Nigeria ni nchi yenye mfumo mzuri wa timu za vijana, na sisi tunaelekea huko huko” amesema Michelsen.
Naye Kocha Mkuu wa Flying Eagles, John Obuh amesema haijui vizuri Ngorongoro Heroes lakini anaiheshimu kutokana na ukweli kuwa inacheza raundi ya pili baada ya kuitoa Sudan katika raundi ya kwanza.
“Sina mchezaji yeyote anayecheza mpira wa kulipwa nje ya Nigeria, lakini tumekuja kushinda ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kucheza raundi ya mwisho na hatimaye tucheze fainali mwakani,” amesema Obuh aliyefuatana na nahodha wake Samuel Okan ambaye ni mlinda mlango.
Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Moses Osano ni sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani wakati VIP B na C itakuwa sh. 5,000. Kiingilio kwa VIP A ni sh. 10,000.
Osano atasaidiwa na Peter Keireini na Elias Wamalwa wakati mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Thomas Onyango. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Charles Masembe kutoka Uganda.