SIMBA YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI AJALI YA MV SKAGET


 
                                                                                                                    19/07/2012
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MSIBA WA KITAIFA
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, kwa niaba ya uongozi, wanachama na wapenzi wa klabu hiyo, wanatoa salamu za rambirambi kwa wananchi wote ambao kwa namna moja au nyingine wameguswa na tukio la ajali ya boti ya Skaget iliyotokea huko Chumbe, Zanzibar.
Rage amesema katika kipindi hiki ambacho wananchi wa Tanzania wako katika msiba mzito, Simba SC inapenda kuwapa pole wote waliokumbwa na msiba huu moja kwa moja na inawaombea kwa Mungu awape moyo wenye subra.
Katika kipindi cha maombolezo, Rage amesema shughuli zote za sherehe zimesimamishwa ndani ya klabu na bendera za klabu zitapepea nusu mlingoti katika kipindi hiki cha siku tatu za maombolezo kama kilivyotangazwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein.
Katika mechi inayofuata ya Kombe la Kagame keshokutwa Jumamosi dhidi ya AS VITA ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wachezaji na viongozi wa Simba watavaa vitambaa vyeusi kama ishara ya kuomboleza msiba huu mkubwa.


AMIR MAFTAH MRISHO
Mchezaji Amir Maftah ambaye jana aliumia katika pambano dhidi ya AS Port ya Djibout amefanyiwa vipimo leo na imebanika kwamba ameteguka (dislocation) kidole chake cha mwisho cha mkono wa kulia.
Kutokana na maumivu hayo, Maftah sasa atakaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki mbili, ikiwa na maana kwamba huenda asicheze kabisa michuano ya Kombe la Kagame inayoendelea jijini Dar es Salaam.
Uongozi wa Simba na jopo lake la utabibu utamtibia Maftah na kuhakikisha anarejea uwanjani mapema na akiwa amepona kabisa tatizo lake hilo.


Mkutano na Waandishi wa Habari
Kesho kutakuwa na mkutano wa waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya Simba mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam. Mkutano huo utafanyika saa sita mchana na mzungumzaji mkuu atakuwa Kocha Mkuu wa Simba, Profesa Milovan Cirkovic.


Mada kuu itakuwa masuala ya kiufundi katika michuano ya Kagame.


Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC

Post a Comment

Previous Post Next Post