MECHI
mbili za nusu fainali ya michuano ya Kombe la Kagame, zinapigwa leo huku
mabingwa watetezi, Yanga wakikabiliwa na kibarua kigumu cha kuwang’oa maafande
wa APR ya Rwanda , mechi
itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam .
Hiyo
itakuwa nusu fainali ya pili, baada ya kuwashuhudia waalikwa AS Vita ya DR
Congo iliyowatupa nje ya michuano hiyo Atletico ya Burundi wakikwaana dhidi ya Azam
FC, inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
Yanga
chini ya Kocha Mkuu Mbelgiji Tom Sainfiet, itakutana na APR ikiwa ni siku
chache tangu wakutane kwenye mechi ya mwisho ya hatua ya makundi na wakali hao
wa Jangwani kushinda mabao 2-0.
Hata
hivyo, Yanga hawapaswi kubweteka kwani timu hizo zilikutana huku zote zikiwa na
tiketi ya robo fainali, hivyo ilikuwa ni mechi ya kukamilisha ratiba hadi
Warwanda hao kupumzisha nyota wake kadhaa.
Yanga
ambao msimu ujao hawatacheza michuano ya kimataifa baada ya kumaliza msimu
uliopita wakiwa nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Azam, watakuwa na kazi ya
kupigania ushindi na hatimaye kutetea taji hilo.
Wakati
Yanga wakitaka kushinda mechi ya leo na hatimaye kutwaa ubingwa wa michuano
hiyo kwa mara ya tano, APR wanataka kuubeba kwa mara ya kwanza baada ya miaka
mitano.
Yanga
ikibeba taji hilo mwaka 1975, 1993, 1999 na 2011, APR wana rekodi ya kujitwisha
mara mbili, 2004 na 2007.
Aidha,
wakati Yanga ikitinga hatua hiyo baada ya kuwang’oa mabingwa wa soka wa
Zanzibar, Mafunzo kwa penalti 5-3, APR iliwafungasha virago URA ya Uganda kwa
mabao 2-1.
Kwa
mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka (TFF), Boniface Wambura, kiingilio
cha kushuhudia mechi za leo kitakuwa shilingi 5,000; 7,000; 15,000 na
20,000.
Alisema,
mechi ya kwanza kati ya Azam na AS Vita, itaanza majira ya saa 8 kamili mchana
kabla ya Yanga kuwakabili maafande wa APR itakayoanza saa 10 jioni.