Wachezaji wa Yanga wakishangilia leo; Picha/habari kwa hisani ya http/bongostaz.blogspot.com |
YANGA imefuzu kuingia Nusu Fainali ya Klabu Bingwa ya soka
Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, baada ya kuifunga Mafunzo ya
Zanzibar kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Wawakilishi wa Zanzibar Mafunzo walikuwa wa kwanza kupata
bao lililofungwa na Ali Othman Mmanga, dakika ya 34, akiunganisha kona ya Juma
Othman Mmanga na Yanga wakasawazisha dakika ya 46, mfungaji Said Bahanuzi
‘Spider Man’.Yanga sasa itamenyana na APR ya Rwanda, keshokutwa ambayo katika Robo Fainali ya kwanza, imeitoa URA ya Uganda kwa kuifunga 2-1, mabao yake yakifungwa na Jean Claude Iranzi dakika ya tisa na Suleiman Ndikumana dakika ya 34, wakati la Watoza Ushuru wa Kampala, lilifungwa na Robert Ssentongo dakika ya 57.
Katika mchezo huo, Juma Othman Mmanga alipoteza fahamu na kuwaweka roho juu wachezaji wenzake na mashabiki, akatolewa nje akipepewa na hakuweza kuendelea na mchezo, lakini taarifa za baada ya mchezo zilisema anaendelea vizuri.
Kipa wa Yanga Berko aliumia dakika ya 69 na akatibiwa kwa dakika tatu, kabla ya kutolewa nje dakika ya 72, nafasi yake ikichukuliwa na Ally Mustafa Barthez ambaye ukaaji wake mazuri langoni wakati wa penalti ulimfanya Said Mussa Shaaban wa Mafunzo akapiga nje na kuipa Yanga ushindi.
Saidi Bahanuzi alipiga penalti ya kwanza, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ya pili, Hamisi Kiiza ya tatu, ya nne Haruna Niyonzima na Athumani Iddi ‘Chuji’ alipiga ya mwisho na kuwainua maelfu ya mashabiki wa Yanga Uwanja wa Taifa.
Yanga SC; Yaw Berko/Ally Mustafa, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Stefano Mwasyika/Idrissa Assenga, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na Rashid Gumbo/Jerry Tegete.
Mafunzo; Khalid Mahadhi Hajji, Ismail Khamis Amour/Hajji Abdi Hassan, Said Mussa Shaaban, Salum Said Shebe, Ali Othman Mmanga, Juma Othman Mmanga/Sadik Habib Rajab, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Jaku Juma Jaku, Mohamed Abdulrahim, Wahid Ibrahim/Kheir Salum Kheir na Ally Juma Hassan.