AZIM DEWJI AZING'ATA SIKIO SIMBA NA YANGA


MWANACHAMA maarufu wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Azim Dewji amezishauri klabu kubwa za Simba na Yanga nchini kuanza kuutumia mtaji wa wanachama wake kujijenga kiuchumi, na kuepuka kuwa tegemezi.
Dewji, ambaye ni mmoja wa wafanyabiashatra maarufu nchini, alisema kwamba kila klabu ina zaidi ya wafuasi milioni 15 nchi nzima, lakini ajabu klabu zinaendelea kuwa ombaomba.
“Huu ni mtaji mkubwa sana, lakini utashangaa klabu haina hata asilimia moja (150,000) ya wanachama wa kweli. Kila siku utasikia wanachama 3,000 hadi 6,000. Kiongozi wa klabu anachaguliwa na wanachama wasiofika 2,000?
“Jamani, kwa klabu inayoshabikiwa na mamilioni ya watu inashindwaje kujijenga kiuchumi kwa kuwatumia mashabiki wake waliozagaa kila kona ya nchi? Jiulize, kama angalau hao watu 150,000 tu wakilipa ada ya mwaka ya 12,000 ambayo hata hivyo bado ni ndogo, si wanaweza kuvuna sh
bilioni 1.8 kwa mwaka, hizi si fedha nyingi?
“Kuna haja ya kufanya mapinduzi ya kweli, badala ya kufikiria kuifunga Simba au Yanga na kutwaa ubingwa wa Bara. Timu yenye uchumi imara, ndiyo inayokuwa na jeuri ya kuwa na kikosi imara na hivyo kufanya vizuri zaidi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Huko ndiko tunakopaswa kwenda,” alisisitiza.
Aidha, Dewji ameipongeza Yanga kwa kufanikiwa kutetea ubingwa wa michuano ya Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame mwishoni mwa wiki, baada ya kuizamisha Azam kwa mabao 2-0 katika mchezo mkali wa fainali kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Dewji, aliyewahi kuifadhili Simba na kuifikisha fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, alisema pamoja na yeye kuwa `Simba Damu’, ana kila sababu za kuimwagia sifa Yanga kwa kuwa imezika haraka matatizo yake na kugeukia kusaka maendeleo.
“Huwezi kuamini kama Yanga iliyopigwa 5-0 na kuibua tafrani nzito Jangwani, ndiyo hii ya leo. Wameikubali hali na kubadilika ndani ya muda mfupi sana. Wana amani na matunda yake yameonekana ingawa walikuwa na kipindi kifupi cha kusuka timu na kurejesha mshikamano ndani ya klabu.
“Naipongeza Yanga na hasa Mwenyekiti wake, Yussuf Manji kwa sababu naamini imani ya wanachama juu yake ndiyo iliyorekebisha hali haraka, naye kama kiongozi kuhakikisha usajili makini unafanyika, kocha anapatikana na uzalendo ndani ya Yanga unarejea,” alisema Dewji.
Aliongeza kuwa, pamoja na matunda ya haraka ya uongozi wa Manji, wana-Yanga wanapaswa kumpa ushirikiano ili kuiondoa Yanga katika utegemezi wa miaka nenda rudi, huku akisisitiza Manji hatabaki Yanga milele.
“Wana kiongozi shupavu, sasa washirikiane naye kuujenga uchumi wa klabu. Haya mambo ya kutegemea mtu kila kukicha si mazuri. Na hili si kwa Yanga tu, hata Simba na klabu nyingine zinapaswa kujikita katika kujijenga kiuchumi ili ziwe na jeuri ya fedha bila ya kutegemea mifuko ya mwanachama mmoja mmoja,” alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post