Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
WAKATI mabingwa wa ligi kuu
soka Tanzania Bara, Simba wakipanga kumuuza nyota wake wa Zambia kwa dau la walau hata dola.20,000
hatma ya wachezaji watakaoichezea timu
hiyo katika msimu ujao wa ligi na michuano ya kimtaifa ipo mikononi mwa kamati
ya utendaji ya klabu hiyo.
Aidha, uwezekano wa kumuacha
nyota wake Salim Kinje iliyemsajili kutoka klabu ya AFC Leopards ni mdogo, huku
mshambuliaji wake wa kimataifa Kanu Mbiyavanga akikalia kutu kavu kutokana na
kucheza mpira wa kufuata kelele za jukwaani.
Habari za uhakika toka klabu
hiyo yenye maskani yake mitaa ya Msimbazi zinaeleza kwamba kamati ya utendaji
ya klabu hiyo imeitisha kikao cha dharura kwa ajili ya kujadili mustakabali
mzima wa wachezaji wa timu hiyo.
Kiongozi mmoja wa kamati ya
utendaji aliliambia Tanzania Daima jana kwamba kikao hicho kitafanyika wakati
wowote katika siku mbili hizi ambapo wanasubiri ujio wa Mwenyekiti wao Alhaj
Ismail Aden Rage ambaye yupo Dodoma
akihudhuria vikao vya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Alisema kikao hicho
kitajadili mapendekezo ya kamati ya ufundi ya klabu hiyo iliyowasilishwa mezani
na ndipo yatakapotolewa maamuzi na nani ataichezea Simba, nani ataachwa na nani
atauzwa au kupelekwa kwa mkopo.
Kiongozi huyo alisema Sunzu
ambaye klabu ya Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeonyesha nia
ya kutaka kumnunua hawatosita kufanya hivyo kwani kwa sasa kiwango chake
hakikidhi mahitaji ya klabu hiyo.
“Suala la Sunzu kidogo lina
ugumu kwani bado ana mkataba na Simba sasa kama
tutaamua kumuacha (kuvunja mkataba) itabidi tumlipe fedha nyingi ndiyo maana
tunaona tumuuze hata kwa dola 20,000,”alisema kiongozi huyo.
Kuhusiana na Kinje, kiongozi
huyo alisema bado ananafasi ya kuitumikia timu hiyo kwani ni mchezaji mzuri
isipokuwa hajachezeshwa katika nafasi anazozimudu ambazo ni namba nne na tano.
“Pia kuna wachezaji kama Lino Masombo, Haruna Shamte hawana nao
walipendekezwa kuondolewa sasa tutakapokutana tutajua zaidi maana ni muhimu
kuangalia ni nani anaisaidia timu na nani mzigo”,aliongeza .