Kocha Mkuu
wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema wanaipa umuhimu mkubwa mechi ya mwisho ya
mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia kwa lengo ni kuhakikisha wanamaliza
wakiwa wa pili katika kundi hilo.
Mechi hiyo
itachezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul, Gambia ambapo Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premiem Lager imeondoka alfajiri ya leo kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Dakar, Senegal.
Kim amesema
wanataka kushinda ugenini, kwani licha ya kuwa wameshatolewa lakini ushindi
utawaongezea pointi kwa ajili ya viwango (rankings) vya Shirikisho la Kimataifa
la Mpira wa Miguu (FIFA) na pia kuepuka kuanzia ngazi ya awali ya mechi za
mchujo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa fainali za 2015.
“Tunacheza
mechi hii tukiwa katika mazingira magumu, kwani wengi wa wachezaji wa kikosi
cha kwanza ni majeruhi. Sijawahi kukutana na hali hii tangu nilipoanza
kuifundisha Taifa Stars, lakini tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri,”
amesema Kim.
Amesema kwa
mipango ya timu yake mechi hiyo ni muhimu tofauti na wengi wanavyofikiria, na
uamuzi wake wa kumwita beki Henry Joseph amezingatia mambo mengi ya kiufundi
ikiwemo nafasi anayocheza na uzoefu wa mchezaji aliyekuwa akicheza nchini
Norway katika klabu ya Kongsvinger IL.
Wachezaji
majeruhi katika kikosi hicho ni Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Aggrey Morris,
Salum Abubakar, Athuman Idd na John Bocco
Vilevile
wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu hawatakuwemo kwenye safari baada ya
klabu yao ya TP Mazembe kutuma taarifa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) leo mchana ikidai ni wagonjwa.
Wachezaji
wanaoondoka kwenda Banjul ni Juma Kaseja, Mwadini Ali, Ali Mustafa, Amri
Kiemba, David Luhende, David Mwantika, Erasto Nyoni, Frank Domayo, Haruni
Chanongo, Henry Joseph, Jonas Mkude, Juma Liuzio, Khamis Mcha, Mrisho Ngasa,
Nadir Haroub, Said Dilunga, Simon Msuva na Vincent Barnabas.