Kamati ya
Uchaguzi imepitisha majina ya waombaji 40 kati ya 58 kwa ajili ya uchaguzi wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPL
Board) utakaofanyika mwezi ujao.
Waliopitishwa
katika orodha hiyo ya awali kwa upande wa Bodi ya Ligi ni Hamad Yahya Juma
(Mwenyekiti) na Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti).
Kwa upande
wa Kamati ya Uendeshaji (Management Committee) ni Kazimoto Miraji Muzo na Omar
Khatib Mwindadi. Walioondolewa kwa vile si wenyeviti wa klabu za daraja la
kwanza kama kanuni zinavyotaka ni Michael Njuweni Kaijage, Salum Seif Rupia na
Silas Masui Magunguma.
Kanda namba
moja (Kagera na Geita) aliyepitishwa kuwania nafasi ya ujumbe Kamati ya
Utendaji ya TFF ni Kaliro Samson wakati Abdallah Hussein Musa ameondolewa kwa
kutojaza fomu ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi.
Jumbe
Oddessa Magati, Mugisha Galibona na Vedastus Lufano wamepitishwa kuwania ujumbe
kupitia Kanda namba mbili (Mara na Mwanza). Samwel Nyalla ameondolewa kwa
kutojaza kikamilifu fomu namba 1 ya maombi ya kugombea uongozi wa TFF kwa
kutoonesha malengo yake.
Waliopitishwa
katika Kanda namba tatu (Shinyanga na Simiyu) ni Epaphra Swain a Mbasha Matutu
wakati Stanslaus Nyongo ameondolewa kwa kukosa sifa ya uongozi wa angalau
uzoefu wa miaka mitano kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF.
Kanda namba
nne (Arusha na Manyara) wamepitishwa wote watatu; ambao ni Ali Mtumwa, Elley
Simon Mbise na Omar Walii Ali. Kanda namba tano (Tabora na Kigoma) nao
wamepitishwa wote; Ahmed Idd Mgoyi na Yusuf Hamis Kitumbo.
Blassy
Kiondo amepitishwa peke yake kuwania ujumbe Kanda namba sita (Katavi na Rukwa)
huku Ayoub Nyaulingo aliondolewa kwa kutokuwa na uzoefu uliothibitika wa miaka
mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.
Naye
Nazarius Kilungeja, Kamati ilikataa maombi yake ya kugombea ujumbe kutokana na
vitendo vyake visivyo vya kimichezo ambavyo kwa kiasi kikubwa vilisababisha
migogoro kwenye Mkoa wa Rukwa, hivyo suala lake litawasilishwa kwa Kamati ya
Maadili kwa ajili ya hatua zaidi.
Kanda namba
saba (Iringa na Mbeya) waliopitishwa ni David Samson Lugenge, John Exavery
Kiteve na Lusekelo Elias Mwanjala. Cyprian Kuyava hakupitishwa kwa vile hana
uzoefu wa uongozi kwa mujibu wa Katiba ya TFF huku Ayoub Shaib Nyenzi
akiondolewa kwa kushindwa kuthibitisha uraia wake.
Elliud Peter
Mvella ameondolewa kwa kushindwa kuheshimu Kanuni za Uwajibikaji wa Pamoja
(collective responsibility) baada ya kushiriki kufanya uamuzi ndani ya Kamati
ya Utendaji ya TFF bila ya kutaka msimamo wake wa kupinga uwekwe kwenye
muhtasari na baadaye kuupinga uamuzi huo akiwa kwenye uongozi wa mkoa. Suala
lake limewasilishwa katika Kamati ya Maadili kwa ajili ya hatua zaidi.
Waliopitishwa
kuwania ujumbe kupitia Kanda namba nane (Njombe na Ruvuma) ni James Patrick
Mhagama na Stanley William Lugenge wakati Kamanga Tambwe ameondolewa kwa vile
alipatikana na hatia ya kushiriki kwenye tuhumu za rushwa kwa waamuzi na
kufungiwa na TFF.
Kanda namba
tisa (Lindi na Mtwara) waombaji wote watatu wameptishwa. Waombaji hao ni
Athuman Kingome Kambi, Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder. Pia
waombaji wote wa Kanda namba kumi (Dodoma na Singida), Hussein Zuberi Mwamba,
Stewart Ernest Masima na Charles Komba wamepitishwa.
Waombaji
wanne kati ya watano wamepitishwa kwa Kanda namba 11 (Morogoro na Pwani).
Waliopitishwa ni Farid Mbarak, Geofrey Nyange, Juma Abbas Pinto na Twahil Twaha
Njoki.
Riziki Juma
Majala ameondolewa kwa vile akiwa mtendaji mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Pwani (COREFA) alishindwa kusimamia Kanuni za Ligi kwa kuruhusu timu
ambayo si mwanachama wa wanachama wa COREFA kucheza ligi, hivyo kusababisha
mgogoro mkubwa kiasi cha mwananchi mmoja kufungua kesi ya kusimamisha Ligi ya mabingwa
wa Mikoa (RCL). Suala lake litawasilishwa Kamati ya Maadili kwa ajili ya hatua
zaidi.
Kanda namba
12 (Kilimanjaro na Tanga) wamepitishwa waombaji wote wawili. Waombaji hao ni
Davis Elisa Mosha na Khalid Abdallah Mohamed.
Waombaji wawili kati ya watano wamepitishwa kuwania ujumbe kupitia Kanda
namba 13 (Dar es Salaam).
Wagombea
wawili kati ya watano wamepitishwa kuwania ujumbe kupitia Kanda namba 13 (Dar
es Salaam). Wagombea hao ni Alex
Crispine Kamuzelya na Muhsin Said Balhabou.
Walioondolewa
ni Omar Isaack Abdulkadir kutokana na vitendo vyake vya kutoheshimu na
kutotekeleza maagizo ya TFF kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF.
Atapelekwa katika Kamati ya Maadili kwa hatua zaidi.
Shaffii
Kajuna Dauda ameondolewa kwa kutumia nyaraka ya mawasiliano baina ya FIFA na
Rais wa TFF bila idhini na kuiweka hadharani kwenye ukurasa wake wa mtandao wa
kijamii, hivyo kukiuka maadili kwa kumiliki nyaraka ambazo hazikuwa kwenye
mamlaka yake. Suala lake linapelekwa katika Kamati ya Maadili.
Naye Wilfred
Kidao ameondolewa kwa kutumia nyaraka za Kamati ya Utendaji ya TFF bila ridhaa
ya kamati, hivyo kukosa uadilifu. Suala lake linawasilishwa kwenye Kamati ya
Maadili kwa hatua zaidi.
Kwa upande
wa nafasi ya Makamu wa Rais, waombaji wote watatu wamepitishwa. Waombaji hao ni
Imani Omari Madega, Ramadhan Omari Nassib na Wallace John Karia.
Athuman
Jumanne Nyamlani na Jamal Emil Malinzi wamepitishwa kuwania nafasi ya Rais.
Omari Mussa Nkwaruro ameondolewa kwa kuwasilisha cheti chenye utata, hivyo
kukiuka utashi wa Ibara ya 27(7) ya Katiba ya TFF. Pia aliwasilisha taarifa za
uongo kuhusu uzoefu na kukiuka Kanuni za Maadili, hivyo suala lake linapelekwa
Kamati ya Maadili.
Naye Richard
Julius Rukambula ameondolewa kwa hakukidhi matakwa ya kugombea uongozi kwa
mujibu wa Ibara ya 12(2)(e) ya Katiba ya TFF inayokataza masuala ya mpira wa
miguu kupelekwa katika mahakama za kawaida. Hivyo naye anapelekwa katika Kamati
ya Maadili kwa hatua stahiki.