TIMU ya soka
ya Tusker inayoshiriki Ligi Kuu nchini Kenya inatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ajili ya kuwakabili miamba ya soka nchini
Simba na Yanga, imefahamika.
Tusker
inatarajiwa kucheza na mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga jumamosi kabla ya
Jumapili kuwakabili Simba ambapo michezo yote itafanyika katika uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Ofisa Habari
wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) iliyoandaa michezo hiyo Mohammed
Mharizo alisema maandalizi ya michezo hiyo yanakwenda vema.
Alisema
lengo la kuandaa michezo hiyo ni kuzipa maandalizi timu hizo hususani katika
kipindi hiki ambapo ligi imesimama kwa ajili ya kuipisha timu ya Taifa ‘Taifa
Stars’ ambayo ipo katika maandalizi ya mechi yake ya Mchujo wa kombe la Dunia
dhidi ya Gambia utakaopigwa ugenini Septemba 7.
Mharizo
aliongeza kuwa tusker inatarajiwa kuja na nyota wake wote kwa ajili ya michezo
hiyo ambapo kama ilivyo kwa Simba na Yanga, itawasaidia na wao kujinoa kwa
ajili ya ligi ya kwao.
Wakati Simba
itautumia mchezo huo kujiandaa na mechi yake dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa
Septemba 14 katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga itakuwa inajinoa
kwa mechi yake dhidi ya Mbeya City utakaofanyika Septemba 14 katika Uwanja wa
Sokoine mjini Mbeya.
Kwa upande
wa Tusker, itakuwa na kibarua kigumu cha ligi ya kwao ambapo inatarajiwa
kucheza na Gor Mahia,Septemba 15.