Msanii wa muziki wa kizazi kipya aliyejijengea
heshima kubwa Tanzania Benard Paul maarufu kama Ben Pol anatarajiwa kuungana na
wasanii wengine kibao katika kupagawisha wakazi wa mji wa Kahama kwenye tamasha
la ‘Kili Music Tour 2013’ tarehe 7 Septemba 2013 katika uwanja wa taifa wa
Kahama.
Ben Pol anayetamba na kibao chake cha ‘Jikubali’
ni mmoja wa washindi wa tuzo za Kili Music Awards 2013 na ataungana na wasanii
wengine tisa kutoa burudani ya kihistoria, “Ninachoomba kwa wakazi wa Kahama
wafurike kwa wingi katika tamasha hilo ambalo tumejipanga kutoa burudani
kikwetu kwetu kabisa, na itakuwa burudani ambayo haijawahi kufanyika Kahama,”
alisema.
Kati ya wasanii wanaotarajiwa kuungana nae
katika tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Jumamosi hii ni pamoja na Linex, Kala
Jeremiah, Prof Jay, Roma Mkatoliki, Fid Q, Izzo Bizness, Recho, Lady Jay Dee na
Barnaba.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja
wa bia ya Kilimanjaro Bw George Kavishe alisema “Tunashukuru
kuwa wasanii wamepokea tamasha hili kwa moyo mkunjufu kabisa na walishiriki
kikamilifu kwenye mikoa yote tuliyopita na tuna ahidi kutoa burudani kali zaidi
katika mikoa iliyobakia,” Alisema Bw Kavishe.
“Nafurahi sana kuona jinsi wasanii wetu wa bongo flea walivyo na vipaji
vikubwa kabisa.Burudani iliyofanyika mpaka sasa ndani ya tamasha la Kili Music
Tour ni la simulizi kwenye mikoa yote tuliyopita! Hii inanipa sana moyo kwamba,
wasanii wamepokea tamasha hili na kuona kuwa kazi ya Tuzo za muziki za Kili ya
kuendeleza vipaji imefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana,"alisema Kaviushe