MAREKEBISHO YA KANUNI ZA UCHAGUZI ZA TFF



Kwa mujibu wa Katiba ya TFF ibara ya 34 (k), Kamati ya Utendaji ya TFF imefanya marekebisho madogo ya Kanuni za Uchaguzi za TFF na za Wanachama wake. Mabadiliko haya yamelenga:
1.Kuainisha kwa uwazi idadi ya siku zinazotakiwa kuzingatiwa na Kamati za Uchaguzi kwa kila shughuli muhimu ya mchakato wa uchaguzi ili kuondoa uwezekano wa kuchelewesha utekelezaji wa hatua mbalimbali za msingi za mchakato wa uchaguzi.
2.Kuweka wazi sifa na matakwa kwa wajumbe wa Kamati za Uchaguzi katika ngazi ya TFF, wanachama wa TFF na Wilaya, kwa lengo la kuondoa ukiritimba wa uongozi na mzozo wa masilahi (Conflict of interest) na pia kubainisha wazi matakwa ya kutofungamana (neutrality) na shughuli za utendaji kwa wajumbe wa Kamati za uchaguzi, ili kuimarisha uwajibikaji katika vyombo vya usimamiaji wa upatikanaji wa viongozi bora wa soka nchini.
Kwa mujibu wa marekebisho yaliyofanyika, Wajumbe wa Kamati za uchaguzi hawataruhusiwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji TFF, Kamati za Utendaji za wanachama wa TFF na za vyama vya mpira wa miguu vya wilaya. Aidha wajumbe wa Kamati za uchaguzi kwa ngazi yoyote hawataruhusiwa kuwa wajumbe wa Kamati za Uchaguzi wa ngazi za chini yake. Pia Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya mwanachama wa TFF hataruhusiwa kuwa mjumbe wa kamati ya uchaguzi ya mwanachama mwingine wa TFF kwa wakati mmoja.
3.Kuondoa utata (ambiguity) katika matakwa ya sifa ya elimu kwa wagombea uongozi katika vyama vya soka nchini. Wagombea uongozi kwa nafasi zote za kuchaguliwa wanatakiwa kuwa na cheti cha kidato cha nne au kuwa na elimu ya kiwango cha zaidi ya kidato cha nne, kwa mujibu wa katiba.
4.Kuweka wazi mtiririko wa ukataji rufaa kutoka ngazi ya Wilaya hadi Taifa (TFF) kwa kuzipa mamlaka Kamati za Uchaguzi za Mikoa kusikiliza rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati za uchaguzi za Wilaya.
5.Kuainisha viwango vya ada za fomu za kuomba uongozi na za rufaa kwa ngazi za Wilaya, Mikoa na TFF.
Kamati inawataka wanachama wote wa TFF kuteua wajumbe wa Kamati za Uchaguzi na kufanya chaguzi zake kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za TFF.


Deogratias Lyatto
MWENYEKITI
KAMATI YA UCHAGUZI –TFF

Post a Comment

Previous Post Next Post