KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF),
imewafungia baadhi ya wachezaji, viongozi na waamuzi kwa utovu wa nidhamu na
ukiukwaji wa taratibu za mashindano.
Katibu Msaidizi wa TBF, Michael Maluwe, amesema utovu huo wa nidhamu ulifanywa na wahusika wakati wa michuano ya Kombe la Taifa, iliyofanyika
mwishoni mwa mwaka jana ambapo Kamati ya
Utendaji iliyoketi hivi karibuni jijini Dar es Salaam ilitoa maamuzi hayo baada
ya kikao chake cha kupitia ripoti za michuano mbalimbali .
Alisema viongozi watatu wa Mkoa wa Shinyanga Ibrahimu Rushemeza, Henry Kizinja
William na Tito Nyalalu wamefungia mwaka mmoja kwa lugha za kebehi,
vitisho na matusi kwa watendaji wa TBF, pamoja na kulazimisha na kushawishi timu zigomee michuano katika vikao
halali.
"baada ya mechi viongozi hao
walivuruga taratibu za kikao
wakishinikiza kulipwa fedha, hivyo hawataruhusiwa kushiriki au kuongoza timu
ndani na nje ya nchi"Alisema.
Alisema, kamati hiyo pia ilijadili hali iliyotokea katika
uwanja wa Leaders ya Kocha Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza, Amri Mohamed, kutokana
na kufanyika vitendo vya utovu wa nidhamu walipocheza na Unguja.
Alisema pamoja na Mwanza kugomea mechi ya kusaka
mshindi wa tatu kwa wanaume, pia ilikaidi adhabu iliyopewa na TBF baada ya kuvunja kanuni za michuano hiyo kuhusu usajili wa
wachezaji ambapo waliingiza wachezaji wa timu yao uwanjani wakati wa mchezo wa
fainali huku timu mbili husika katika mchezo huo zikijiandaa kukaguliwa.
"Kitendo hicho kiliashiria kuleta vurugu na uharibifu wa
amani ya mchezo mbele ya mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, hivyo kuitwa polisi wa ziada kulinda
usalama.
Kutokana na vitendo hivyo, mkoa na viongozi wa Mwanza wamefungiwa mwaka mmoja kushiriki michuano yoyote itakayoandaliwa na TBF, huku katika kipindi hiki cha adhabu viongozi hao
hawataruhusiwa kushiriki au kuongoza ama kujishulisha na mpira wa kikapu katika
michuano yoyote, kliniki za mpira wa kikapu, michuano ya shule kitaifa,
kushiriki mikutano yoyote ya wadau nchini na nje ya nchi.
Kama hiyo haitoshi adhabu hiyo imekwenda pia kwa wachezaji Juma Kisoky, Willison Masanja, Shilinde Francis, Amon Sembelya Mohamedi Ally,
Amri Mohamedi, Kizito Bahati, Ahmed Said, Adam Jegame, Bundala, Charles, Chacha
Tubet, Shinda Vincent, Enock Charles na Kocha Robert Mwita.