MWIGIZAJI, mtayarishaji
mahiri wa filamu nchini na balozi wa Zuku Swahili Movie, Aunt Ezekiel, amesema
kuwa ataendelea kuilinda rangi ya ngozi yake kwa kutotumia vipodozi vikali
‘mkorogo’ ili kuwa mweupe.
Akizungumza hivi karibuni,
msanii huyo alisema kuwa, anachokifanya yeye ni kujua aina ya vipodozi
anavyostahili kutumia, lakini si vile vya kumbadili, ikiwamo rangi ya ngozi
yake.
Msanii huyo, aliyasema hayo
wakati akizungumzia juu ya kuteuliwa kwake pamoja na Jacob Stephen ‘JB’ kuwa
mabalozi wa king’amuzi cha Zuku kwa upande wa wasanii, inayojulikana kwa jina
la Zuku Swahili movie.
“Kwa kweli ninashukuru kwamba,
sijawahi wala sitarajii kutumia mkorogo ili niwe mweupe, ninaridhika na ngozi
yangu na naamini ndiyo inayonifanya niwe kipenzi cha wengi na ningewaomba
wasichana kote nchini, ambao hawajatumia wasithubutu, kwani kuna madhara
makubwa,” alisema.
Msanii huyo alisema kuwa,
anaamini Zuku Swahili Movie, itawasaidia kukuza soko la kazi zao, kwa kuwa
itakuwa ikionesha zaidi filamu nyingi za Kitanzania, kutoka Swahiliwood pamoja
na tamthilia, vichekesho, kwaya na kazi zingine za sanaa zinazotumia Lugha ya
Kiswahili kutoka nchi za Afrika Mashariki.