Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
wachezaji (ambayo katika uamuzi huu itarejewa kama ‘Kamati’) iliyokutana Julai
17 mwaka huu, baada ya kupitia mikataba na nyaraka zote zinazohusiana na
mchezaji Kevin Yondani katika kujiridhisha juu ya hadhi yake ya usajili katika
mashindano ya Kombe la Kagame kama
zilivyowasilishwa mbele yake imefikia uamuzi ufuatao;
1. Kwa mujibu wa mapitio ya nyaraka zote
zilizotajwa hapo juu na kufanyiwa upembuzi yakinifu, Kamati iliridhika pasi na
shaka yoyote kuwa suala zima la mchezaji Kevin Yondani ni la kiutendaji, hivyo
uamuzi wa Sekretarieti ya TFF kuwasiliana na Klabu ya Simba kwa suala hilo la
kiutendaji kama Sekretarieti ilivyofanya katika barua yake ya Julai 14
mwaka huu ulikuwa sahihi.
2. Kamati ilibaini kuwa Mkataba wa mchezaji
Kevin Yondani na Klabu ya Simba ulimalizika Mei 31 mwaka huu. Hivyo kwa
taratibu za usajili mchezaji Kevin Yondani kuanzia Juni 1 mwaka huu alikuwa ni
mchezaji huru.
3. Aidha Kamati ilibaini kuwa Mkataba
uliowasilishwa na Klabu ya Simba TFF ukiwa na maana ya kuongeza mkataba
uliokuwepo TFF baina ya mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya Simba uliwasilishwa
TFF, Juni 7 mwaka huu ambapo ni kinyume cha utaratibu wa kuongeza mikataba ya
wachezaji unaozitaka klabu kuwasilisha mikataba ya kuongeza muda wa mikataba ya
wachezaji wao wakati mkataba halisi haujaisha muda wake. Hivyo mkataba huo kwa
jicho la kisheria haupo.
4. Hata kama kamati ingeuona mkataba huo katika
jicho la sheria, bado mkataba huo una tatizo la kisheria hasa katika tarehe ambazo
pande mbili husika ziliingia makubaliano hayo. Ukiuangalia mkataba huo
unabainisha kuwa, wakati mchezaji Kevin Yondani aliingia makubaliano Desemba 23
mwaka jana, upande wa pili wa kimkataba ambao ni Klabu ya Simba inaonekana
iliingia makubaliano hayo kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Geofrey Nyange
Kaburu, Desemba 23 mwaka huu.
5. Kisheria utata huu unaweza kuondolewa na
pande husika tu kwa kurekebisha dosari hiyo kwa maridhiano kuweka saini katika
mabadiliko hayo ili kuthibitisha mabadiliko hayo. Hivyo katika jicho la
kisheria mkataba huo hauwezi kutumika kumzuia mchezaji huyo kwenda katika klabu
anayoipenda wakati akiwa huru.
Kutokana na maelezo yote hapo
juu, Kamati imeridhia hatua iliyochukuliwa na Sekretarieti ya TFF ya kumruhusu
mchezaji Kevin Yondani kuichezea timu ya Yanga katika mashindano ya Kombe la
Kagame 2012.
Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati ya Sheria, Maadili na
Hadhi za Wachezaji
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)