KIPIGO cha mabao 3-1
ilichokipata timu ya Simba kutoka kwa timu ya Azam katika michuano ya Kombe la
Kagame, kiliibua mjadala mzito bungeni kwa mashabiki wa klabu hiyo kupigwa
vijembe na wenzao wa Yanga.
Shabiki mkubwa wa
Simba, Profesa Juma Kapuya ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Magharibi, ndiye
alianza kuchokoza mjadala pale alipoitwa na Mwenyekiti wa Bunge ili awasilishe
taarifa ya Kamati yao
ya Miundombinu.
Prof. Kapuya baada ya
kufika mbele, alisimama na kutaka kuanza kuzungumza bila kuwasha kipaza sauti,
akidai rangi yake nyekundu ambayo inatumiwa na klabu yake kuwa inamchanganya,
jambo lililoibua vicheko kwa wabunge wenzake.
Hata hivyo, baada ya
kipindi cha maswali na majibu kwisha wakati wa asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge,
Jenista Mhagama, aliwatambulisha wageni na kutoa matangazo ya kazi kisha
akawaambia wabunge kuwa ana tangazo fupi kwao.
“Waheshimiwa wabunge
nataka kuwajulisha kuwa Kampuni ya Azam ina bidhaa nyingi na nzuri, hivyo
mnashauriwa kutumia bidhaa hizo kwa kuwa ni imara na bora, maana hata mashabiki
wa Simba wanajua kwamba Azam ni kiboko,” alisema Mhagama na kuibua vicheko kwa
wabunge.
Hata hivyo Profesa
Kapuya alipomaliza kusoma taarifa ya kamati, alihitimisha kwa vijembe kwa
watani zao wa Yanga akisema: “Nawapongeza Simba kwa kucheza vizuri japo
wamefungwa na Azam, lakini wamekubali, hawajawa kama
wenzetu waliofungwa goli tatu na timu hiyo halafu wakapigana…na sasa wamepewa
jina la ‘HU HAA’.