KOMBE la ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame jana liligeuka kuwa dili baada ya
mashabiki wa klabu hiyo kutozwa sh 2,000 ili kupiga nalo picha.
Yanga ilitwaa ubingwa huo wa pili mfululizo Jumamosi
iliyopita baada ya kuitandika Azam FC mabao 2-0 katika mchezo wa fainali
uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kutokana na furaha za ubingwa huo baadhi ya mashabiki
wamekuwa wakimiminika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Jangwani na Twiga kwa
lengo la kupiga picha ya kumbukumbu na kombe hilo.
Hata hivyo mashabiki hao wamejikuta wakitozwa kiasi
hicho cha fedha na mtu anayeendesha zoezi la upigaji picha hizo.
“Ni kweli mashabiki wanatozwa kiasi hicho cha fedha
kwa ajili ya kupiga picha na kombe,” alisema Ofisa Habari wa Yanga, Louis
Sendeu.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa timu hiyo,
Mbelgiji Tom Saintfiet amewapa mapumziko ya siku nne wachezaji wa timu hiyo
mara baada ya kazi ngumu ya kushiriki michuano ya Kagame na kufanikiwa
kulibakisha kombe Jangwani.
Saintfiet alisema kutokana na hatua hiyo wachezaji hao
hawana budi kupata mapumziko ya siku hizo na hatimaye Ijumaa wataanza rasmi
maandalizi yao ya Ligi Kuu Bara.