WAKATI mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba
wakianza mazoezi jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mserbia Milovan Circovick
anatarajiwa kurejea nchini kesho.
Milovan anarejea kutoka kwao Serbia alikokwenda kwa
mapumziko mafupi baada ya timu yake ya Simba kutolewa kwenye michuano ya Kombe
la Kagame wiki iliyopita katika hatua ya robo fainali.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel
Kamwaga, baada ya kurejea, Milovan ataanza kuisuka timu yake kwa Tamasha la
‘Simba Day’ litakalofanyika Agosti 8.
“Ni matarajio yetu kocha atarejea hiyo Jumatano kama
ilivyopangwa ili aweze kuendelea na programu yake ya kukinoa kikosi,” alisema.
Alisema, wachezaji wote wa Simba jana asubuhi walianza
mazoezi ufukweni kabla ya jioni kuhamia viwanja vya TCC, Chang’ombe.
Aidha, Kamwaga alisema maandalizi ya mkutano mkuu wa
mwaka wa klabu hiyo uliopangwa kufanyika Agosti 5 kwenye Bwalo la Maofisa wa
Polisi, Oyesterbay yanakwenda vema.
Alisema kila mwanachama anayetaka kushiriki mkutano huo anapaswa kuwa hai, hivyo alipie
kadi kuepuka usumbufu siku ya mkutano.