NI YANGA NA AZAM FAINALI KAGAME

Na Prince Akbar
BAO pekee la mwanasoka bora wa Uganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ dakika ya 110, jioni hii limeipa Yanga tiketi ya kucheza Fainali ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo, na sasa itamenyana na Azam FC keshokutwa, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kiiza alifunga bao hilo, kwa kichwa akiunganisha krosi ya karibu ya Haruna Niyonzima ambaye alitumia mwanya wa mabeki wa APR kuzubaa wakisikilizia maamuzi ya refa, baada ya Kiiza kuangushwa.
Yanga waliinuka na wakaanzisha shambulizi la haraka lililozaa bao hilo. Dakika tatu baada ya bao hilo, beki wa Yanga, Godfrey Taita alitolewa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na sasa ataikosa fainali.
Ikumbukwe mwaka jana, Yanga iliifunga Simba SC katika fainali bao 1-0 na kutwaa taji la nne la michuano hiyo, baada ya awali kutwaa Kombe hilo 1975, 1993 na 1999.
Mapema katika Nusu Fainali ya Kwanza, Azam FC iliitoa AS Vita kwa kuifunga mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na John Bocco ‘Adebayor’ na Mrisho Ngassa, wakati la Vita ya DRC lilifungwa na Mfongang Alfred.
Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul/Shamte Ally/Juma Seif, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Godfrey Taita, Haruna Niyonzoma, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na David Luhende.
APR; Jean Ndoli Claude, Olivier Karekezi, Suleiman Ndikumana, Mugiraneza Jean, Johnson Bogoole, Lonel St Preus, Ngabo Albert, Iranzi Jean Claude, Mbuyu Twite, Dan Wagaluka na Tuyizere Donatien.

Post a Comment

Previous Post Next Post