Mkuu wa masoko na mawasiliano wa Vodacom, Kelvin Twisa
KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom imejivunia udhamini wake kwa ligi kuu soka Tanzania bara na kusema umeleta manufaa makubwa katika maendeleo ya mchezo huyo.
Akizungumza juzi katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa ligi hiyo, mkuu wa masoko
na mawasiliano wa Vodacom Kelvin Twisa alisema kampuni yake imetoa zaidi
ya shilingi milioni 113 kama zawadi za washindi hao na hivyo kufanya mwaka huu
zwadi kuongezeka tofauti na mwaka jana zilikuwa shilingi milioni 90.8.
“Tunajivunia kuwa wadhamini wa ligi kuu bara ambapo vipaji
vingi vimeonekana na viwango vya kuvutia pia katika mechi zote na ndio maana
hii leo tupo katika kutoa zawadi kwa washindi,”alisema.
Katika halfa hiyo, ilitambulishwa tuzo mpya inayohusisha
wachezaji vijana waliofanya vema kwenye timu hizo ambapo waliotwaa ni pamoja na
Rashid Mandawa (Coastal Union), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting) na Frank Damayo
aliyekuwa anaichezea JKT Ruvu na sasa amesajiliwa Yanga ambapo kila mmoja
alizawadiwa shilingi milioni moja.
Azam Fc ilifanikiwa kuongoza kwa kutwaa tuzo tano ikiwemo
ile ya nafasi ya pili iliyowapatia sh.mil.22, timu yenye nidhamu (mil.7.8),
kocha bora-Stewart Hall (mil.3.8), mfungaji bora- John Bocco (mil.3.9) na
mchezaji bora- Aggrey Morris (mil.3.3).
Aidha mabingwa Simba walitwaa mil.50, huku kipa wake Juma
Kaseja alitwaa tuzo ya kipa bora na kuzawadiwa Mil.3.3, wakati Yanga
ilizawadiwa mil.15 kwa kushika nafasi ya tatu na Martin Sanya alitwaa tuzo ya
mwamuzi bora na kuzawadiwa mil.3.8.
Ligi kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012 ilianza kutimua vumbi
Agosti 20,2011 na kumalizikia Mei 6, 2012 na kuvishirikisha vilabu 14
vikiwemo Simba, Yanga, Azam Fc, African
Lyon, Kagera Sugar, Mtibwa Sugara, Toto Africans, Moro United, JKT Ruvu, Ruvu
Shooting, Coastal Union, Polisi Dodoma na Oljoro JKT.