Na Dina
Ismail
TANZANIA ni moja ya nchi zinazoaminika na kusifika kuwa na
watu wenye amani, upendo na ushirikiano.
Kweli! tunasifika kwa hilo toka kwa watu wa nje,
lakini kwa kiasi kikubwa hali hiyo haipo baina yetu katika baadhi ya makundi ya
kijamii.
Tukiangalia katika sekta
ya sanaa na michezo suala la kutowathamini watu hao lipo na
linaendelea kushika kasi kila kukicha.
Hapa kwetu,msanii
au mchezaji anakuwa anathaminiwa au
kupendwa pindi anapokuwa mzima wa afya
na mwenye nguvu zake.
Tofauti na
nchi za wenzetu ambazo hata kama zina machafuko lakini wasanii na wanamichezo
wanathaminiwa katika hali zote mradi tu amepata kutoa mchango wa kisanaa na
michezo katika nchi yake.
Kwamba, kwa Tanzania thamani ya wasanii na
wachezaji inaonekana pindi wanakuwa
katika uzima na afya njema lakini
wakipatwa na ugonjwa au umauti hakuna anayejali.
Tumeshuhudia
mara kwa mara taarifa za wasanii na wanamichezo kuomba msaada wa matibabu
wanapopata maradhi lakini mapokeo ya maombi yao huwa si ya kuridhisha.
Matokeo yake
jukumu la kuuguza hubaki kwa wanafamilia na kwa bahati mbaya kuna wanaofikwa na
umauti au kilema kutokana na maradhi yao na hakuna anayejali.
Kama hiyo
haitoshi, kuna baadhi ya wachezaji wamejikuta wakikatiza ndoto zao baada ya
kuumiwa wakizitumikia timu zao na bila huruma wanatelekezwa bila msaada
wowote kubaki wakijiuguza wenyewe.
Hili
linasikitisha sana, kwani pamoja na mchezaji kuumia akiwa chini ya himaya yako
bado unamuacha akahangaike kujitibia mwenyewe sasa hapo thamani yake iko wapi.
Kwamba,
utaona ufahari kujitokeza katika msiba wake na kutangaza kuwasilisha kiasi
kadhaa cha ubani,hilo hata mungu hapendi kwani kama mlikuwa mnamthamini
mngemuhudumia kuanzia mwanzo mpaka pale ahadi yake itakapofika.
Hebu tuachane
na roho za kikatili kwa watu wetu hawa kwani kwa namna moja ama nyingine
wanasaidia kuitangaza nchi, wanasaidia kukupa wewe kula, wanasaidia kukupa wewe heshima, wanatoa burudani, wanaelimisha
na mengineyo mengi.
Pamoja na
yote mazuri na michango yao katika jamii lakini hatuwathamini kama
inavyostahili kulingana na waliyoyafanya wakati wa uzima au uhai wao.
Kama hiyo
haitoshi, kuna wengine wanakumbwa na umauti na hata timu, taasisi au kundi
alilokuwa akilifanyia kazi linashindwa hata kuhudhuria katika msiba wake.
Basi
umeshindwa kuhudhuria msiba, mfano mchezaji huyo alipata kuwa tegemeo katika
timu yako na kucheza kwa mafanikio leo anazikwa na timu yako inacheza lakini
unashindwa hata kusimama kwa dakika moja tu kumuombea.
Watanzania
tubadilike kwa kuthamini na kujali wenzetu!