Na Dina
Ismail
LIGI kuu
soka Tanzania bara inaelekea ukingoni
ambapo mshike mshike upo katika makundi
mawili, zile zinazowania ubingwa wa msimu wa 2016/17 na zenye kupambana na
kushuka daraja.
Katika mbio
za kuwania ubingwa, vigogo vya soka nchini Simba na Yanga ndizo zinazopambana
kuwania ubingwa wa ligi hiyo, huku Majimaji, Toto Africans,JKT Ruvu na Mbao Fc
zikiwa katika mchuano wa mojawapo kujikwamua kubaki Ligi kuu kwani timu tatu za
mwisho zitashuka.
Msimu mpya
wa ligi 2017/2018 utazikaribisha timu za Singida United (Singida), Lipuli
Fc na Njombe mji zote kutoka mkoani
Iringa ambako timu hizo kwa sasa zimeshaanza maandalizi kwa na namna moja ama
nyingine.
Singida
United na Lipuli Fc si mara yao ya kwanza kushiriki katika ligi hiyo ambako
mara ya mwisho zilishiriki ilikuwa miaka 17 iliyopita na kisha kushuka daraja.
Njombe mji
yenyewe yenye maskani yake katika mji wa Njombe mkoani Iringa hii itakuwa mara
yake ya kwanza kushiriki katika ligi kuu.
Kwa
wanaofuatilia historia ya soka la bongo na hasa Ligi Kuu ni wazi kwamba
wanazifahamu sana Singida United na Lipuli na hiyo inatokana na umahiri wao
ilizokuwa nazo enzi zinashiriki ligi hiyo.
Tuseme ni
bahati mbaya tu kwao ilipelekea kushuka daraja lakini ni timu ambazo zilikuwa na wachezaji wenye
vipaji vya hali ya juu kiasi ambacho vigogo vya soka nchini Simba na Yanga
ziliweza kuvuna wachezajaji kutoka huko kwa nyakati tofauti.
Kwa sasa
timu hizo zipo katika maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu na ili kuweza
kushiriki vyema tayari zimeanza mikakati madhubuti ya kuimarisha vikosi v yake,
benchi la ufundi na miundombinu yake, yaani viwanja vya mazoezi.
Timu ya
Singida United kwa kuonesha kuwa imejipanga vema kushiriki kikamilifu tayari
imefanya maboresho kwenye benchi lake la ufundi kwa kumuajiri aliyepata kuwa
kocha na Mkurugenzi wa benchi la Yanga, Hans Van Der Pluijm.
Kama hiyo
haitoshi, Singida United pia imeanza usajili wake kwa kuwasajili wachezaji watatu
wa kimataifa kutoka Zimbabwe, Tafadzwa
Kutinyu, Elisha Muroiwa na Wisdom
Mtasa.
Singida
United pia ipo katika ukarabati wa hali ya juu wa Uwanja wa Namfua ambao itautumia
katika ligi hiyo kama uwanja wake wa nyumbani.Zoezi hilo linafanywa na Chama
cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida.
upandaji wa
nyasi huku ikielezwa ifikapo Agosti mechi zote za nyumbani zitachezwa uwanjani
hapo.
Singida
United ambayo imemwajiri kocha mpya Mholanzi, Hans Pluijm na kusajili wachezaji watatu wa kigeni ni
miongoni mwa timu tatu zilizopanda daraja kushiriki ligi kuu msimu ujao pamoja
na Njombe Mji na Lipuli FC.
Kwa upande
wa Lipuli Fc, ambayo iko chini ya Chama cha soka Mkoa wa Iringa (IRFA)
iliyochukua jukumu la kuiendesha klabu hiyo kutokana na kuwepo kwa mgogoro uliozuka ndani ya uongozi wa klabu
hiyo,nayo ipo katika mipango ya kujiweka sawa ili kushiriki vema katika ligi
hiyo.
Njombe Mji
Fc ambayo inanolewa na kocha maarufu nchini, Hassan Banyai nayo imedhamiria
kuhakikisha inashindana na si kushiriki kwenye ligi hiyo kubwa nchini.
Kwa mantiki
hiyo, timu hizo zitacheza ligi hiyo kiushindani zaidi na si kufanya bora liende
na hasa ikizingatia zilifanya juhudi na jitihada kubwa kuhakikisha zinapanda
hadi ligi hiyo.
Kwamba, ziwe
mfano kwa timu nyingine zinazopanda kwa kufanya vema na hata ikiwezekana
mojawapo itwae ubingwa au hata kuingia tatu bora mwishoni mwa ligi.
Ushiriki wao
usiwe nguvu za soda kwa kuishia kuzifunga tu Simba na Yanga halafu mechi nyingine
zinapoteza, zitakuwa zimewakosea sana wananchi na pia kupoteza nguvu, heshima
na jitihada bure za wakazi wa miji ya Iringa na Singida ambao walikuwa nazo
bega kwa bega mpka zinapanda.
Aidha, ni
vema timu hizo zikajiepusha na siasa za Simba na Yanga, kuanzia katika usajili
na hata kipindi watakachoanza kushiriki Ligi Kuu, zicheze soka la ushindani
kama zilivyofanya katika Ligi daraja la kwanza.