Na Dina
Ismail
MIAKA ya
nyuma shindano la Miss Tanzania lilikuwa
likichukuliwa kama uhuni kiasi cha
wazazi kukataza watoto wao kushiriki.
Lakini
kadiri miaka ilivyosonga ndipo wazazi walianza kulikubali shindano hilo kwa
kuruhusu watoto wao baada ya kuona mafanikio waliyoyapata baadhi ya warembo
mara baada ya kushiriki shindano hilo.
Miss
Tanzania ‘beauty with purpose’ ni zaidi ya shindano kwani mrembo anaweza
asishinde taji kuu lakini akanufaika kutokana na ushiriki wake.
Kwa mantiki
hiyo kuna baadhi ya wadada ambao walipata kushiriki shindano hilo leo hii
wamejijengea heshima kubwa katika jamii kutokana na kazi wanazozifanya, lakini
heshima inaanzia kushiriki kwao Miss Tanzania.
Kihistoria
shindano hilo kwa hapa nchini lilianza rasmi mwaka 1960 na mrembo wa kwanza
kutwaa taji hilo alikuwa Theresia Shayo ambaye sasa hivi ni marehemu.
Hata hivyo
kutokana na maadili na utamaduni wa Tanzania serikali ililifuta mwaka 1967
kabla ya kurejeshwa tena katika miaka ya 1990 na ndipo hapo Tanzania ilianza
kupata mafanikio kupitia mashindano ya urembo.
Mrembo Aina Maeda ndiye alikuwa mrembo wa kwanza
tangu kurejeshwa kwa mashindano hayo ambapo alitwaa taji hilo mwaka 1994 yakiwa
chini ya uratibu wa Hashim Lundenga.
Mashindano
hayo yalianza kwa kuendeshwa kimkoa na kadiri miaka ilivyosogea wigo wake
ulitanuka na kufikia kufanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara, wilaya,
vitongoji na hata katika ngazi ya vyuo
vya elimu ya juu kulisakwa washiriki.
Kupitia
mashindano hayo, pamoja na zawadi nono za nyumba, magari pamoja na mamilioni ya
fedha, tumeshuhudia warembo mbalimbali wakijipatia umaarufu ambao uliwawezesha
kupata kazi katika makampuni mbalimbali, mikataba katika makampuni mbalimbali
ya matangazo na mengine mengi.
Hawa ni
baadhi ya warembo waliopitia Miss Tanzania na sasa hivi wanaheshimika kutokana
na kazi wanazozifanya sambamba na mchango wao mkubwa katika jamii:
Hoyce Temu:
Huyu ni Miss
Tanzania mwaka 1999 ni mrembo ambaye amekuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya zaidi shughuli za kijamii kwani tangu atwae taji hilo jina lake
limebaki kuwa juu kila uchwao.
Mrembo huyo
licha kipindi chake cha mwaka mmoja cha kufanya kazi za kusaidia jamii kama
Miss Tanzania lakini ameendelea kuifanya hivyo hadi sasa ambapo kupitia kipindi chake cha Televisheni
cha ‘Mimi na Tanzania’ amekuwa akiongea na watu wenye shida mbalimbali na
kuwaombea misaada kwa wasamaria.
Hoyce ambaye
kwa sasa anafanya kazi kitengo cha mawasiliano na Mahusiano katika ofisi za
Umoja wa Mataifa (UN) nchini Kwa kutambua huduma yake kwa jamii, aliwahi
kutajwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga kama mlimbwende
bora kuliko wote.
Nancy Sumari:
Alitwaa taji
la Miss Tanzania 2005, pia taji la Miss World Afrika mwaka huo.
Ni mrembo
mwingine msomi na anayeheshimika hapa nchini kutokana na utumishi wake katika
jamii.
Nancy ni
mfanyabiashara, pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Bongo Media, pamoja na
Mfuko wa The Neghesi Sumari
Foundation.Pia ni mtunzi wa kitabu cha hadithi za watoto kiitwacho, Nyota Yako.
Jacqueline Ntuyabaliwe ‘K-Lyn’:
Ni mrembo
aliyetwaa taji mwaka 2000.Kabla ya kushiriki shindano alikuwa akijihusisha na
uimbaji wa muziki katika bendi ya Tanzanite.
Baada ya
kumaliza kulitumikia taji lake aliendelea kuwa msanii ambako alitoa singo zake
kama msanii wa kujitegemea huku vibao vyake kama Crazy Over You, Nipe mkono, Best
na nyinginezo ambazo zilimpatia umaarufu zaidi.
K-Lyn ambaye
ni mke wa mfanyabiasha maarufu nchini Reginald Mengi kwa sasa amejikita zaidi
katika biashara akimiliki duka la liitwalo Amorette ambalo linatengeza na kuuza
thamani za ndani pamoja na upambaji wa ndani.
Jokate Mwegelo:
Jina lake
lilianza kusikika zaidi mwaka 2006 aliposhika nafasi ya pili katika shindano la
Miss Tanzania, huku taji hilo likitwaliwa na Wema Sepetu.
Jokate
alitwaa taji la balozi wa kinywaji cha Redd’s kilichokuwa mmoja ya wadhamini wa
shindano hilo ambapo aliweza kufanya kazi mbalimbali zilizohusiana na mitindo
na ubunifu kama balozi.
Baada ya
muda wake kumalizika Jokate alionekana kupenda zaidi masuala ya mitindo ambapo
alijikita katika sekta hiyo, sambamba na kujihusisha na uigizaji na muziki.
Kwa sasa
Jokate amejikita zaidi katika biashara chini ya Lebo yake aliyoipa jina la
Kidoti ambapo ameshaingiza sokoni bidhaa zake kadhaa ikiwemo nywele, mabegi ya
shule na kandambili.
Aidha, mrebo
huyo pia anaendesha kampeni yake iitwayo ‘Be Kidotified’ inayohamasisha
wanafunzi wenye vipaji mbalimbali kutojiweka nyuma.
Happiness Magesse ‘Millen’:
Jina lake
linang’ara duniani kwa sasa kupitia fani ya mitindo.
Alitwaa taji
la Miss Tanzania mwaka 2001 na baada ya kumaliza muda wake alikwenda nchini
Afrika Kusini na kuanza kujihusisha na kazi ya mitindo ambayo anaifanya mpaka
sasa.
Millen
ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani pia anamiliki mfuko wake uitwao ‘Millen
Foundation’ ambao ni mahususi kwa kuendesha kampeni maalum ya kuelimisha
wasichana juu ya ugonjwa wa Endomitriasis ambao huwasababishia maumivu makali
wakati wa siku zao za hedhi.
Hao ni
baadhi kwani wapo warembo wengi tu
waliopitia katika shindano hilo ambao wanafanya mambo makubwa ya
kueleweka katika jamii.