KOCHA MICHO AWATAKA WATANZANIA WAMPE MUDA POULSEN

MICHO

Na Mwandishi Wetu, Cairo

KOCHA wa zamani wa Yanga, Sredojevic Milutin 'Micho', amesema ni vyema Watanzania wakampa muda Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen ili aijenge timu, kwani namna alivyoiona kuna kazi kubwa inahitajika ili ilete matunda mazuri.Amesema ni vigumu kuamini namna Taifa Stars inavyocheza kama ilikuwa na kocha mmoja kwa miaka minne, badala yake inaonekana ni timu mpya na yenye kocha anayeanza moja kufundisha, hivyo matunda yake yatachelewa kuonekana.Alitoa kauli hiyo juzi mjini hapa, baada ya kumalizika mchezo wa kuwania nafasi ya tano kati ya timu ya Taifa Stars na Sudani katika michuano ya soka Nchi za Bonde la Mto Nile Uwanja wa Al Salam na Stars kulala mabao 2-0 yote yakifungwa kipindi cha pili.Micho ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa El Hilal ya Sudan, hakumtaja kwa jina lakini kocha aliyekuwa kabla ya Poulsen ni Mbrazil Marcio Maximo aliyefika Tanzania Julai 2006 na kuondoka Julai 2010 na Poulsen raia wa Denmark alirithi mikoba Agosti mwaka jana na amesaini mkataba wa miaka miwili.Desemba mwaka jana Poulsen aliiongoza timu ya Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' kutwaa Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, wakati Maximo Januari mwaka juzi aliiongoza Taifa Stars kucheza fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zilizofanyika Ivory Coast na kuishia hatua ya makundi."Niwe mkweli katika hili, Tanzania ina safari ndefu sana kufikia kwenye mafanikio, Watanzania ni marafiki zangu, nimeishi nao vizuri, mpaka kesho nikienda wananipokea vizuri, lakini timu yao inahitaji muda sana kujengwa, wampe muda mwalimu, ni kocha mzuri na ana uzoefu wa kutosha atawasaidia," alisema.Alisema Stars sasa ndiyo inaanza kujengwa upya, inaonekana si timu ya ushindani na haioneshi kama kweli ilikuwa na kocha mmoja kwa miaka minne mfululizo, badala yake kinachoonekana ni timu mpya na kocha mpya anaanza kuijenga.Micho yupo mjini Cairo na El Hilal iliyoweka kambi kujiandaa na michuano ya kimataifa na alisisitiza hasemi kocha aliyekuwepo Stars kabla ya Poulsen ni mbaya, lakini Stars haionekani kama ilikuwa ikinolewa na kocha mmoja kwa miaka minne.Michuano ya soka Nchi za Bonde za Bonde la Mto Nile ilitarajiwa kumalizika jana usiku kwa mchezo wa fainali kati ya wenyeji Misri na Uganda, ambapo Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zenyewe zilicheza kuwania mshindi wa tatu. Burundi imeshika nafasi ya saba kati ya timu saba.Wakati huo huo, Poulsen akizungumza juzi baada ya vijana wake kufungwa mabao 2-0 alisema kuna makosa waliyafanya sehemu ya ulinzi na ndiyo yaliiangusha timu yake na kuruhusu mabao kipindi cha pili.Hata hivyo alisema soka ndivyo lilivyo, lakini hakuwa tayari kuzungumzia kwa ujumla kufanya vibaya kwa timu katika michuano hiyo au kitu gani ilichopata kiufundi na kusema atafanya hivyo akishafika Dar es Salaam na kujipanga vizuri.Timu itaondoka Cairo leo saa tano usiku na inatarajiwa kufika Dar es Salaam saa 11 ikiwa imeshika nafasi ya sita kati ya tmu saba zilizoshiriki michuano hiyo, ambayo bingwa amejinyakulia zaidi ya sh. milioni 200 za Tanzania, wa pili zaidi ya sh. milioni 170 za Tanzania na wa tatu zaidi ya sh.milioni 130 za Tanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post