KUANZIA sasa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) litawajibika
kulipa kiasi cha shilingi milioni 10 kwa uharibifu wa idadi yoyote ya viti
utakofanywa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam .
Hatua hiyo inafuatia kukithiri kwa uharibifu wa viti hivyo
ambao umekuwa ukifanywa na mashabiki wa soka hapa nchini na hasa wa Vilabu vya
Simba na Yanga.
Akizungumza jana kwa niaba ya Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, mkurugenzi wa Idara ya Michezo nchini Leonard Thadeo
alisema kwamba lengo la kufanya hivyo ni kudhibiti vitendo vya uharibifu wa
viti katika Uwanja huo.
Alisema fedha hizo zitalipwa bila kujali idadi ya viti hata
kiwe kimoja au kumi kwani serikali imesikitishwa na kitendo cha muendelezo wa
vurugu kwenye uwanja huo kwani kinawadhalilisha wanamichezo wote wa Tanzania na
jumuiya ya Kimataifa.
Thadeo aliongeza kuwa uharibifu huo umekuwa ukifanyika mara
kwa mara na serikali imekuwa ikilazimika kufanya matengenezo bila kuwahusisha
wadau wengine lakini inaonekana kujengeka kuwa tabia miongoni mwa baadhi ya
mashabiki hatua ambayo haiwezi kuvumilika.
“Inasikitisha kuona hata baadhi ya viongozi wa vilabu vyetu
hawatambui kuwa wanawajibu wa msingi kama
viongozi kuwaelimisha wanachama na
wapenzi wa vilabu vyao kuacha uharibifu badala yake wanadai kuwa viti vingi
viliharibika,kaharibu nani? alihoji Thadeo.