Na Dina Ismail
BAADA ya
kutoshiriki Ligi Kuu soka Tanzania Bara kwa takribani miaka 17, hatimaye timu
ya Lipuli ya Iringa imekata tiketi ya kucheza ligi hiyo msimu wa 2017/18.
Lipuli iliyokuwa tishio katika miaka ya nyuma kwenye
soka, imekata tiketi hiyo baada ya kufikisha pointi 29 ambazo haziwezi kufikiwa
na timu yoyote katika kundi A huku ikibakiwa na michezo miwili.
Chini ya
kocha wake mkuu, Richard Amatre ambaye ni raia wa Uganda, timu hiyo ilianza
kuonesha dalili za kupanda daraja tangu kuanza kwa ligi hiyo ambapo iliweza
kufanya vema katika michezo yake.
Amatre
ambaye alipata kuwa kocha msaidizi wa Simba, amekuwa akijigamba kwa timu yake
kufanya vema na kweli ndicho kilichotokea na hivyo kuifanya timu yake kupanda
daraja.
Kocha Amatre
ambaye amedumu na timu hiyo kwa miaka mitatu pamoja na kuwapongeza wachezaji
wake kwa hatua hiyo anasema haikuwa rahisi kwao kuibuka vinara katika kundi
lao.
Lipuli
ambayo miaka ya nyuma ilipokuwa ikishiriki Ligi Kuu Bara ilikuwa ni moja ya
timu tishio sana, haijapanda kirahisi kwani kabla ya mwaka huu ilikuwa ikiishia
nafasi ya pili na tatu.
Ni moja ya
timu iliyokuwa na heshima kubwa Tanzania; mkoa wa Iringa una matajiri wengi
ambao kama wakiamua wanaweza kuihudumia timu hiyo na kuepuka vishawishi hivyo
vya timu kubwa na kutoa upinzani mkubwa kwa Yanga na Simba zinapokwenda kwenye
uwanja wa Samora pale Iringa.
Enzi hizo,
hakuna mshabiki wa soka aliyekosa kuifahamu Lipuli kwani haikuwa timu ya
kawaida kwa kutandaza kabumbu safi kupitia kwa nyota wake waliokuwa na uwezo wa
hali ya juu.
Kama hiyo
haitoshi, Lipuli ilikuwa ni roho ya Wana Iringa kwani ni timu pekee iliyokuwa
ikiuwakilisha vema mkoa huo, hivyo ni wazi kwamba wakali hao wa zamani
wataendeleza makali yao ya zamani.
Kwamba,
lengo lao la kufanya mapinduzi ya soka kwa mkoa wa Iringa liendane sambamba na
kufanya vema katika Ligi Kuu Bara kwani kinyume na hapo itakuwa ni kazi bure.
Kupanda kwa
Lipuli ni nafasi pekee kwa wakazi wa mkoa wa iringa pamoja na wadau wa soka
kuhakikisha wanaiunga mkoni na kuipa sapoti timu hiyo ili iweze kudumu na siyo
kupanda na kushuka.
Matajiri wa
Iringa wanatakiwa kujitolea kuisaidia timu hiyo iweze kujimudu na kuondokana na
ukata ambao unaweza kuitia timu hiyo majaribuni kwa wachezaji kupokea rusha na
kupeleke timu hiyo kupoteza mwelekeo kwenye ligi ya msimu ujao.
Lakini kitu
kingine ambacho ni chamuhimu zaidi kwa timu hiyo ni kuepuka kufungamana na
upande mmoja katika ya timu mbili kubwa za Simba na Yanga na kujenga timu
isiyofungamana na upande wowote kati ya hizo mbili.
Timu nyingi
kwenye ligi ya Vodacom zimekuwa zikiathirika kwa jambo hilo la kufungamana na
upande mmoja kati ya timu hizo mbili, na hali huwa mbaya na wakati mwingine
kushuka daraja pindi timu kubwa inapohitaji pointi tatu ili kutwaa ubingwa au
nafasi fulani kwenye msimamo .